RAS BALANDYA AZINDUA HUDUMA ZA KIBINGWA AWAMU YA PILI, AWATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza ndugu Balandya Elikana amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wananchi kwa kuboresha huduma za afya hadi kuwasogezea huduma bobezi katika vijiji ili wananchi wasipate adha ya kusafiri kwenda kwenye hospitali za rufaa.
Ametoa shukrani hizo leo Novemba 04, 2024 wakati akizindua huduma za kibingwa na bingwa bobezi awamu ya pili katika hospitali za halmashauri za mkoa huo zitakazofanywa na madaktari wa Dkt. Samia kwa juma moja.
Balandya ametumia wasaa huo kuwaalika wananchi kwenye hospitali zote za wilaya za mkoa huo kuanzia leo Novemba 04, 2024 hadi Novemba 06, 2024 huku akisema kuwa wamesogezewa huduma hadi vijijini hivyo hakuna sababu yoyote ya kutofika kwenye hospitali kupata huduma za kibingwa.
Aidha, amebainisha kuwa wagonjwa zaidi ya milioni 2.6 wamefika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na wengine walipewa rufaa kwenda kwenye hospitali kubwa kwa ajili ya kupata huduma bobezi hivyo ni fursa kwa wananchi kupata huduma hizo katika maeneo yao.
"Huduma za afya zinamgusa mwananchi moja kwa moja, Mwanza tunatambua umuhimu wenu na tunaahidi kuwapa ushirikiano mkunlbwa katika kipindi chote mtakachokuwepo hapa ili msikwame kwa lolote na ni matarajio yetu mtawarithisha wataalamu wetu utaalamu wenu." Balandya.
Mkurugenzi msaidizi huduma za afya za mtoto, mtoto mchanga na vijana kutoka Wizara ya Afya Dkt. Felix Bundala amesema uwepo wao kwenye huduma hizo tangu Septemba 9 mwaka huu wamehudumia wagonjwa elfu 60 katika mikoa 20 kabla ya wiki 2 zilizobaki kukamilisha mikoa yote 26.
"Pamoja na kuwapatia huduma wananchi, tunatambua faida wanayoipata familia wenye wagonjwa na kwa hakika familia zimefutwa machozi katika mazingira tofauti na tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuona umuhimu wa kundi hili kurudia kutoa huduma kwa wananchi wa vijjijini." Dkt. Bundala.
"Mtapokua huko tuna upungufu mkubwa sana wa madaktari bingwa hivyo niwaombe sana mkajitoe hata usiku mtakapohitajika kwani tuna uhitaji mkubwa wa huduma za kibobezi mathalani Sengerema." Dkt. Jesca Lebba, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.