RAS Balandya: Wataalamu wa Kilimo tumieni mafunzo mnayopata ili mkalete mageuzi ya Kilimo- Biashara
Wataalamu wa Kilimo kutoka Mikoa saba wanaondelea kupata mafunzo rejea ya siku mbili Mkoani Mwanza namna ya kuimarisha usimamizi wa huduma za ugani, wametakiwa kuja na mageuzi chanya kwenye sekta ya Kilimo ili kuwa cha kibiashara zaidi.
Rai hiyo imetolewa leo kwenye ukumbi wa Mtakatifu Dominic na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg.Balandya Elikana wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo na kuwahimiza kutimiza malengo ya Serikali ya ukuaji wa asilimia 10 kwenye sekta hiyo Ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Bw.Daniel Machunda amebainisha Serikali ya awamu ya sita imenuia kufanya mageuzi ya Kilimo kwa kutenga fedha nyingi za kuimarisha maeneo yote muhimu ikiwemo nyenzo za usafiri kwa Maafisa ugani.
"Kupitia agenda 10/30 azma ya Serikali ni kuongeza matumizi ya Teknolojia bora za kisasa ikiwemo matumizi sahihi ya pembejeo, kupima afya ya udongo na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji." Machunda
Amewataka wataalamu hao kutumia kikamilifu siku za mafunzo hayo kwa kujadili namna ya kutoa huduma bora za ugani kwa wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani ili kuchangia katika kufikia malengo ya kitaifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za ugani kutoka Wizara ya Kilimo,Bi Upendo Mndeme amesema kuimarisha kwa huduma za ugani ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuendelezwa sekta ya kilimo (ASDP 2) ya kuongeza uzalishaji na tija.
"Ni lazima sasa tutoke kwenye kilimo cha kujikimu na kwenda kilimo biashara na kumfanya huyu mkulima kupiga hatua zaidi kwenye sekta hii ndiyo maana Serikali inahakikisha inafanya jitihada zote hizo kwa vitendo kwa kufanya uwekezaji mkubwa ili kilimo kipunguze umasikini na kujenga uchumi imara," amesisitiza Mndeme.
"Ndugu mgeni rasmi tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha dhamira ya kweli ya kujenga uchumi imara kupitia sekta hii ya Kilimo,wajibu wetu sisi kama viongozi tuliopewa jukumu la kusimamia ni kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa kwa kufanya ufuatiliaji na wakulima wanapata ushauri kwa wakati,"Emil Kasagara Katibu Tawala Msaidizi,Uchumi na Uzalisalhaji.
Kasagara amebainisha licha ya Wizara ya Kilimo kuwawezesha vyombo vya usafiri Maafisa ugani,imeanzisha mfumo wa kidigitali wa M-Kilimo ambao unamuwezesha mkulima kutumia simu za kiganjani kuwasiliana na maagmfusa ugani.
"Teknolojia ya M-Kilimo inawawezesha wakulima kupata ushauri kwa haraka na taarifa za masoko ya mazao ya Kilimo kwa njia ya simu za mkononi,hivyo kupitia mafunzo haya ni wajibu wenu Maafisa ugani kuwafundisha wakulima kutumia mfumo huu ili wapate huduma hizo,"Dkt.Rehema Mdendemi,mwakilishi kutoka TAMISEMI.
Wataalamu hao kutoka ngazi ya Mkoa na Halmashauri wanatoka Mikoa ya Mwanza,Mara,Geita,Kigoma,Kagera,Shinyanga na Simiyu.
Kauli Mbiu ya mafunzo hayo ni "Agenda 1030 Kilimo-Biashata".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.