RAS Mwanza afanya ukaguzi wa miradi ya afya isiyokamilika Sengerema,ataka taarifa ya mchakato wa ukamilishaji wiki hii
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana ametoa maagizo ya kupatiwa taarifa ndani ya siku mbili kuhusu mchakato wa ukamilishaji wa miradi 17 ya afya wilayani Sengerema iliyojengwa kwa nguvu ya wananchi ili hatua za haraka zifanyike wananchi wapate huduma.
Akizungumza jana jumatatu na watendaji wa Halmashauri ya hiyo baada ya kufanya ukaguzi wa miradi iliyo kwenye vijiji tofauti, Balandya ameagiza kupatiwa gharama za umaliziaji zikiwemo na nyumba za watumishi na upatikanaji wa vifaa tiba.
"Mkurugenzi nimeona miradi ya zahanati imeishia hatua ya boma,
kaa na timu yako ya wataalamu mfanye kazi hii kwa umakini na taarifa niipate Ofisini kwangu kabla ya jumatano ili ifanyiwe kazi ngazi husika," amesema Balandya wakati akiwa kijiji cha Nyamasale iliyopo zahanati iliyoishia hatua ya boma.
Akiwa kwenye kijiji cha Nyitundu iliyopo zahanati inayotoa huduma lakini inakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba,nyumba za watumishi na wafanyakazi, Mtendaji huyo wa mkoa amemtaka Mkurugenzi kupatia ufumbuzi haraka wa changamoto hizo ili wananchi wapate huduma bora.
Balandya akiwa kwenye ukaguzi huo kijiji cha Tabaruka ameshuhudia mradi wa zahanati uliofikia hatua ya ujenzi asilimia 38 huku zahanati ya kijiji cha Itonga ikitoa huduma lakini ikikabiliwa na uhaba wa maji na choo hakijakamilika, hapo ametoa agizo la kuchimbwa kisima haraka na ukamilishaji wa choo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imechukua hatua hiyo ikiwa ni utekekezaji wa maagizo ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa baada ya kufanya ukaguzi wa baadhi ya miradi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita na kubaini mapungufu kadhaa, hata hivyo taarifa ya miradi 17 ya afya aliyopatiwa na mbunge wa Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu kuwa imekamilika lakini haitoi huduma haikuwa sahihi baada ya Katibu Tawala wa mkoa kubaini miradi hiyo bado ipo hatua ya awali kabisa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.