Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,Ngusa Samike amefunga wiki ya Huduma za Maabara Mkoani humo kwa kutoa wito kwa vijana kusomea masomo ya Sayansi ili waweze kupata fursa ya kujiajiri na kuajiriwa.
Katibu Tawala huyo amesema mkazo na mazingira mazuri yawekwe Shuleni Vijana wachangamkie masomo hayo kwani bado Taifa linawahitaji aina hii ya Wataalamu wa Huduma za Maabara.
"Kumekuwa na kasumba ya kuamini masomo ya Sayansi ni magumu la hasha! hebu tuanze kubadilika" amesisitiza Katibu Tawala Samike
Aidha amesema taarifa aliyopata ya Wananchi waliojitokeza ni zaidi ya watu elfu mbili waliopata huduma mbalimbali inaridhisha na kuwapa ari wao kama Serikali kujipanga zaidi mwakani.
Amewahimiza Wananchi kuendelea kuona umuhimu wa kupata huduma za kiuchunguzi kabla ya kutumia dawa ili kupata usahihi wa kile wanachotakiwa kutibiwa.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Esther Maliki amesema Wiki ya Huduma za Maabara imekuwa na faida kwa Wananchi kwani wamepata huduma za kiuchunguzi na ushauri, pia chanjo ya Maradhi mbalimbali ikiwemo Uviko 19 na homa ya Ini.
Aidha Mwenyekiti wa Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya Tanzania,Betrand Msemwa amesema upande wa Maradhi yasiyoambukiza kama Kisukari jumla ya Wananchi 238 wamejitokeza na 15 waligundulika na tatizo hilo wakati uchangiaji wa Damu salama waliojitokeza ni watu 64.
Wiki ya Huduma za Maabara huadhimishwa kila mwaka mwishoni mwa Aprili ambapo Mkoa wa Mwanza
ulianza Maadhimisho hayo Mei 2 mwaka huu yakifunguliwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Mhandisi Robert Gabriel.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.