Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike ameipongeza Kamati ya Amani ya Mkoa kwa kuiunga mkono Serikali katika kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi na kutaka iendelee hivyo katika mambo mengine ya Kitaifa.
Akifungua mafunzo kuhusu Sensa inayowashirikisha Viongozi wa Dini kutoka Wilaya za Mkoa wa Mwanza,Ngusa amesema Wananchi wana kila sababu ya kushiriki zoezi hilo kwa Maendeleo ya Taifa letu.
"Mmefanya Jambo zuri kamati ya Amani ya Mkoa kutoa mafunzo haya, Sensa ni muhimu sana kwa Serikali kupanga mipango ya Maendeleo tuna imani Wananchi watahamasika kushiriki kuhesabiwa" amesema Samike
"Nawashauri pia kwenye nyumba zenu za ibada wahamasisheni waumini kwa kuweka mabango yenye ujumbe wa Sensa lengo likiwa wananchi washiriki kikamilifu" amesema Ngusa
Ngusa amesema wapo baadhi wenye uelewa mdogo au kuingia shaka kuhusu Sensa lakini kwa kupeana elimu hii ni fursa nzuri ya kubadilishana uzoefu kati yenu Viongozi wa Dini na Serikali na hatimaye Wananchi watapata uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa Sensa na Makazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza Sheikh Hassan Kebeke amesema mafunzo hayo ni matokeo ya kuitikia wito wa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan wa kuwataka Viongozi wa Dini kuhamasisha Sensa.
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Askofu Charles Sekelwa amebainisha hata maandiko matakatifu yanatufundisha kuhusu Sensa hivyo wajibu wao kama Viongozi wa Dini kuendelea kuwaelimisha waumini wao.
Mafunzo hayo yanawashirikisha Viongozi wa Dini kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza na yanatolewa na Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Joachim Otaru.
Sensa ya Watu na Makazi itafanyika nchi nzima Agosti 23 mwaka huu kwa wale walio lala ndani ya mipaka wa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.