RAS Mwanza atoa rai kwa Wahandisi kusimamia Ubora wa Miradi
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Daniel Machunda amewasihi Wahandisi kusimamia taaluma yao vema na kutekeleza miradi katika ubora unaokusudiwa.
Ametoa wito huo leo Agosti 22, 2023 kwenye Kikao kazi cha Wahandisi, Maafisa Elimu na Waganga Wakuu wa Wilaya kilichoketi kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kufanya tathmini ya changamoto zinazowakabili kwenye utekelezaji wa miradi.
Machunda amesema serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga Miundombinu na kuwaboreshea wananchi huduma hivyo ni wajibu wa wataalamu kusimamia ubora na thamani ya fedha kwenye utekelezaji.
"Twendeni tukajenge miradi iliyo bora, ni lazima tujenge Imani kwa wananchi kwamba serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia ipo kwa ajili ya kuwapa huduma bora sio tunajenga mradi mwaka huu alafu baada ya miaka michache mradi unaharibika." Machunda amefafanua.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Miundombinu, Mbunifu Majengo Chagu Nghoma amefafanua kuwa kikao kazi hicho kimelenga kufanya tathmini ya miradi iliyotekelezwa kwenye mwaka 2022/23 ambapo wameziangazia changamoto walizopitia na kwa pamoja wamebaini namna bora ya kutekeleza kwa siku za usoni.
Aidha, amebainisha kuwa kwa pamoja wamekubaliana kutekeleza miradi kwa ushirikiano ili kuhakikisha Wahandisi na idara watumiaji wanakuwa sehemu ya utekelezaji na kuitunza miradi kwa faida ya vizazi vya sasa na miaka ya baadae.
Vilevile, mbunifu majengo Nghoma amefafanua kuwa kwenye kikao kazi hicho wameihusisha Ofisi ya TAKUKURU ambayo imetoa wito kwa wataalamu hao kuwa wazalendo kwa kuzingatia kunakua na thamani ya fedha iliyokusudiwa kwenye miradi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.