RAS MWANZA ATOA RAI KWA WARATIBU TASAF KUTUMIA MFUMO WA MANUNUZI KWA UFANISI
*Aagiza kutatuliwa kwa changamoto zote ili Mfumo wa NEST utumike ipasavyo*
*Atoa wito kwa Maafisa hao kutoa taarifa za uaminifu kwa walengwa kwa wakati*
*Asema Mwanza imepokea zaidi ya Bilioni 91 kuanzia Julai 2015 kwa wanufaika*
*Ataka wafuatiliaji kuwa wazalendo katika kuwafikia walengwa na wanufaika*
*Asema zaidi ya miradi 174 ya zaidi ya Bilioni 33 imetekelezwa Mwanza*
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amewataka Waratibu na watendaji kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) kuzingatia Sheria na Kanuni za Matumizi ya Mfumo wa Manunuzi (NEST) na Utoaji wa taarifa ili kuwahudumia walengwa kwa ufanisi.
Balandya amebainisha hayo mapema leo Februari 21, 2024 wakati akifungua Kikao kazi cha kujadili maendeleo ya Utekelezaji wa Mpango wa TASAF na Matumizi ya Mfumo wa Manunuzi (NEST) na Mfumo wa Taarifa wa TASAF kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
"Mfumo wa Ununuzi na Mfumo wa Utoaji taarifa wa TASAFni muhimu sana katika Utekelezaji wa Mradi wa TASAF kwa ujumla wake katika kuhakikisha umasikini unaondoka kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na wafadhili wa mradi huo." Amesema Katibu Tawala.
Aidha, Katibu Tawala huyo amebainisha kuwa Mwanza imepokea zaidi ya Bilioni 91 kuanzia Julai 2015 kwa wanufaika 71,381 huku zaidi ya miradi 174 ya zaidi ya Bilioni 33 ikitekelezwa Mkoani humo tangia uzinduzi rasmi wa mradi huo Mkoani Mwanza mpaka sasa na kwamba fedha hizo ni nyingi zinahitaji uzalendo kwenye usimamizi.
Bi. Haika Shayo, Mkurugenzi wa Uratibu kutoka TASAF amesema wapo Mwanza katika kikao kazi cha kawaida cha kupitia utekelezaji wa shughuli za mradi ili kuhakikisha mradi huo unafanyika kwa ufanisi na kujifunza matumizi ya Mfumo wa Ununuzi katika ngazi ya Halmashauri na Mfumo wa Taarifa wa TASAF.
"Hatuna budi kuwa na taarifa sahihi na za wakati kwa walengwa ili kuhakikisha wanaufurahia na unawahudumia kwa ufanisi hivyo baada ya kikao kazi hiki tunatarajia ufanisi mkubwa zaidi kwa watendaji wetu." Amesema Bi. Shayo, Mkurugenzi wa Uratibu TASAF.
Vilevile, amebainisha kuwepo kwa changamoto ya matumizi ya mfumo wa manunuzi hivyo ni imani yake kwamba kupitia mafunzo hayo ya siku 3 ya uwezeshaji changamoto hiyo itatatuliwa kwani wahusika wote ikiwemo Waratibu, Wahasibu, Maafisa Ufuatiliaji wa Mpango wa TASAF, Maafisa Manunuzi wamehusishwa katika mafunzo haya.
Monica Mahundi, Mratibu wa Mpango wa TASAF Mkoa wa Mwanza amebainisha kuwa jumla ya wanufaika 71,381 wamefikiwa huku Miradi 174 katika Sekta za Elimu, Afya na Miundombinu ya Barabara yenye zaidi ya Bilioni 33 zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.