Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike amewataka Vijana kujitambua wao ni nguvu kazi ya Taifa hivyo wasikubali kuyumbishwa na mabadiliko ya ki-Dunia ambayo baadhi yao wamejikuta yakiwagharimu maisha yao.
Katibu Tawala Ngusa amesema hayo wakati wa Mdahalo Maalum uliohusu Ukatili wa Kijinsia uliofanyika Chuo Kikuu cha Mt.Agustino Mkoani Mwanza,amesema rika la Vijana wengi kuanzia miaka 18 hadi 25 wamekumbwa na majanga ya kila aina kuanzia utumiaji wa Dawa za kulevya na Ngono isiyo salama ambavyo kwa pamoja vimewapotezea ndoto zao za kimaisha.
"Huku vyuoni mambo mengi yasiyo na tija kwenu yanafanyika baadhi yenu mnaishi kama mke na mume,upigaji wa picha za utupu wengine kujiua,haya yote ni lazima mpambane kuyatokomeza kama mna nia njema na maisha yenu"
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT, Prof Hosea Rwegoshora amebainisha kinacho wagharimu Vijana wengi ni tamaa ya kulazimisha kufanikiwa ki-maisha bila kujali wanatumia njia gani sahihi.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoani Mwanza, Faith Lukindo amesema mkazo wa elimu hauna budi kuwekwa kwa Vijana kuanzia ngazi za Shule kutokana na kundi hili kuwa katika hatari zaidi na kasi ya mabadiliko ya ki-dunia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya Wadada, Lucy John amesema kwa kutambua umuhimu wa Vijana katika ujenzi wa Taifa wameamua kuwajengea msingi mzuri wa elimu ya Afya ambayo itawasaidia kupambanua baya na zuri.
Baadhi ya watoa Mada alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike,Mratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Polisi,Faraja Mkinga, Mratibu wa Afya ya Uzazi Mwanza, Bertha Mkinga, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa Faith Lukindo, pamoja na Mhadhiri msaidizi kutoka SAUT, Fides Zakayo.
Mdahalo huo umewashirikisha wanafunzi kutoka baadhi ya Vyuo vilivyopo Mkoani Mwanza na Makundi mengine ya Vijana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.