RAS MWANZA AZINDUA BODI YA USHAURI YA MWACHAS
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg.Balandya Elikana leo Aprili 3,2025 amezindua rasmi Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mwanza (MWACHAS) huku akitoa wito kwa uongozi wa chuo na wadau wa elimu kushirikiana katika kuboresha sekta ya afya kupitia mafunzo bora kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wakati wa uzinduzi huo uliofanyika chuoni hapo eneo la Bugando wilayani Nyamagana, Balandya ameipongeza MWACHAS kwa hatua yake ya kuunda bodi imara ya ushauri akisisitiza kuwa taasisi za elimu zina jukumu kubwa la kuandaa wataalamu wa afya watakaosaidia kuboresha huduma za tiba nchini.
"Tunahitaji kuhakikisha kuwa vyuo vya afya vinakuwa na mifumo madhubuti ya kusimamia ubora wa elimu na mafunzo ili kuzalisha wahitimu wenye weledi wa hali ya juu,"Katibu Tawala
Aidha, ameitaka bodi hiyo kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine ili kutatua changamoto zinazokabili chuo, hususan katika upatikanaji wa miundombinu bora.
"Serikali iko tayari kushirikiana nanyi lakini ni lazima kuwe na mipango thabiti ya maendeleo ili MWACHAS iwe chuo bora kinachotoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa".amesisitiza mtendaji huyo wa mkoa
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw.Isaaka Ndasa amesisitiza kuwa jukumu kuu la bodi hiyo ni kuhakikisha MWACHAS inazidi kupiga hatua na kuwa miongoni mwa taasisi za elimu ya afya zinazoongoza nchini.
"Tutahakikisha tunasimama imara ili kuboresha viwango vya elimu, kufuatilia mwenendo wa chuo na kuhakikisha kwamba chuo chetu kinaendelea kukua",Ndasa
Mwenyekiti huyo pia ametoa wito kwa wanachama wa bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kutimiza malengo ya chuo.
Mkuu wa Chuo, Prof.Hyasinta Jaka ambaye pia ni Katibu wa Bodi hiyo ameiomba Serikali kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili chuo hicho hasa katika eneo la ujenzi wa Chuo katika eneo lililopo karibu na Hospitali ya Wilaya ya Ilemela Mwanza.
Aidha amesisitiza kuwa chuo kina dhamira ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi wake, lakini kinahitaji msaada zaidi ili kuboresha vitendea kazi na kuongeza idadi ya wahadhiri wenye uzoefu.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa elimu, wahadhiri, na wanafunzi wa MWACHAS.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.