*RC Makalla afanya ukaguzi wa Jengo jipya la Abiria la uwanja wa ndege Mwanza,ahimiza ujenzi uendelee haraka
*Ataka TAA wakabidhiwe haraka mradi huo*
*Akiri kuwepo na Changamoto za kiujenzi
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Amos Makalla ameagiza mchakato wa makabidhiano wa Jengo jipya la Abiria la uwanja wa ndege kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwenda kwa Mamlaka ya viwanja vya ndege TAA ufanyike kwa haraka ili waendelee na kazi ya ujenzi.
Mhe.Makalla ametoa kauli leo mara baada ya kufanya ukaguzi wa Jengo hilo linalojengwa kwa kuchangiwa fedha kutoka Serikali kuu,Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza na kusisitiza hakuna sababu ya mradi huo kuendelea kusimama licha ya kuwepo na kasoro nyingi za kiufundi.
"Nimekuja kufanya ukaguzi wa Jengo hili mengi nitazungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa,lakini nichukue nafasi hii kuhimiza TAA ndiyo wenye dhamana na jengo hilo hivyo waachiwe waendelee na ujenzi huu wakishirikiana na Wizara husika ya Ujenzi na Uchukuzi",CPA Makalla
Awali akitoa taarifa ya ujenzi huo ambao
kwa sasa umesimama,Katibu Tawala Msaidizi,Miundombinu Mkoa wa Mwanza Mhandisi. Chagu Nghoma amesema Halmashauri ya Jiji la Mwanza wametoa zaidi ya Shs Bilioni 1.45,Ilemela zaidi ya Shs Bilioni 1.42 na Serikali kuu zaidi ya Shs Bilioni 9.
Aidha Afisa uendeshaji wa uwanja wa ndege Mwanza,Senneth Lyatuu aliyezungumza kwa niaba ya Meneja wa uwanja huo,amebainisha hawana utaratibu wa kuendesha shughuli zao kwa ubia na Taasisi nyingine za Serikali au Halmshauri.
Mhe Makalla ameshauri kuwepo na kikao baina ya pande zote husika zilizochangia fedha hizo ili kuona uwezekano wa kurudishiwa au taratibu nyingine.
Jengo la Abiria la uwanja wa ndege lilianza kujengwa mwaka 2019 kwa agizo la Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt.John Magufuli kwa gharama ya zaidi ya Shs Bilioni 13 na hadi sasa zimetumika zaidi ya Shs Bilioni 9.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.