*RC Makalla afungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mkoa ahimiza weledi kazini*
**Asema atawafuata wananchi walipo kutatua kero zao*
**Ahimiza nidhamu ya kazi*
*Ataka kuona huduma bora kwa wananchi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Amos Makalla amelitaka Baraza la Wafanyajazi kutoka Ofisi yake kuwa mfano wa kuchapa kazi ili wananchi waipate taswira halisi ya Serikali inayohimiza uwajibikaji na kuwajali wananchi wake.
Akifungua leo kikao cha Baraza hilo kilichofanyika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mhe.Makalla amewakumbusha wajumbe kutanguliza maslahi ya Utumishi wenye weledi mahali pa kazi na kuepuka aina yoyote ya kuwakwaza wananchi wanapohitaji huduma.
"Niwakumbushe ndugu zangu wafanyakazi tudumishe nidhamu ya kazi,hii ni pamoja na kuwahi kufika kazini na kutoa huduma bora,sura halisi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa nyie ndiyo mnayoionesha tofauti na hapo hata mimi mtaniangusha na kuonekana siwajibiki ipasavyo",Amesisitiza CPA Makalla.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha yeye siyo mtu wa kukaa Ofisini na badala yake muda mwingi atautumia kukutana na wananchi huko walipo ili kuzijua kero zao na kuzipatia ufumbuzi na kutaka utaratibu huo uwe kwa kila kiongozi.
Awali akitoa taarifa fupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa kulifungua Baraza hilo,Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,Ndg Balandya Elikana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, amesema Baraza hilo lipo kwa mujibu wa Sheria na miongoni mwa majukumu yake ni kuangalia utendaji wa kazi kwa ujumla na haki zote stahili za wafanyakazi zinavyozingatiwa.
"Mhe.Mkuu wa Mkoa kikao hiki cha Baraza cha siku moja tutajadiliana mambo mbalimbali na kuyapatia ufumbuzi ikiwemo bajeti ya Mkoa,changamoto za kupandishwa wafanyakazi madaraja na mikakati ya kuboresha mazingira ya kazi",amesema Mtendaji huyo wa Mkoa.
Wajumbe wa Baraza hilo ni pamoja na watumishi wote wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na makatibu Tawala wa Wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.