RC MAKALLA AHOJI ONGEZEKO LA GHARAMA SHILINGI BILIONI 11 KUPEWA KAMPUNII YA EMIRATES BUILDERS LTD MRADI WA MAJI USAGARA
*Aagiza TAKUKURU kuchunguza mkandarasi aliyeshinda tenda ya awali kwa Shilingi bilioni 21 kukataliwa na kupewa Kampuni ya EMIRATES kwa shilingi Bilioni 32*
*Ataka taarifa ya Uchunguzi huo ikamilike ndani ya siku 14*
*Awataka RUWASA Makao Makuu kutoa ushirikiano kwani wao ndio waliompa mkandarasi EMIRATES Ltd kwa gharama kubwa*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe CPA Amos Makalla ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kuchunguza sababu za mkandarasi aliyeshinda tenda ya awali kwa Shilingi bilioni 21 kukataliwa na kupewa Kampuni ya EMIRATES kwa Shilingi Bilioni 32 kwenye Mradi wa Maji Ukiriguru wilayani Misungwi.
Makalla ametoa agizo hilo mapema leo Novemba 07, 2023 wakati wa ziara yake wilayani Misungwi (Ukiriguru-Usagara) wakati akikagua Mradi Mkubwa wa Maji unaokwenda kunufaisha zaidi ya wananchi elfu 85 kwenye maeneo mbalimbali huku ukitarajiwa kuwa na Matanki Makubwa 4 yenye ujazo wa Lita Milioni 6.5
Mhe. Makalla amehoji ni kwanini Mkandarasi Emirates Builders Limited mwenye gharama za juu za ujenzi kwa ongezeko la zaidi ya Bilioni 11 tofauti na Mkandarasi aliyeshinda awali apewe kazi hiyo na kwamba imepata hofu ya Ukiukwaji wa sheria na taratibu za Zabuni na ndipo akaagiza uchunguzi huku akiwataka kutumia siku 14 kukamilisha zoezi hilo na taarifa aipate.
Aidha, ametoa wito kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Makao Makuu kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi huo kwani wamesimamia taratibu za kumpata mkandarasi huyo aliyepatikana kwa gharama za juu tofauti na makampuni mengine yaliyohitaji kazi hiyo kwa Bilioni 19 na 21 lakini wakaamua kumpatia mwenye gharama za juu.
Vilevile, ametumia wasaa huo kuwataka RUWASA kusimamia vizuri mradi huo ukamilike ndani ya muda uliopangwa wa miaka miwili hadi februari 2025 na amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kujenga mradi huo kwani hadi sasa zaidi ya Bilioni 5 zimeshatolewa na mradi umefikia asilimia 12 ya utekelezaji wake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.