RC MAKALLA AIPONGEZA BENKI YA TIB KWA KUCHOCHEA MIRADI YA UCHUMI
*Amewaomba wadau wa benki TIB kuwekeza katika Hoteli kukuza utalii, kuwekeza katika Uvuvi, Kilimo na Madini ni maeneo yenye tunu katika kukua kiuchumi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ameipongeza Benki ya Maendeleo nchini (TIB) kwa kuchochea uchumi kupitia mitaji ya kibiashara na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali hususani za Utalii, Madini, Biashara na Usafiri, Kilimo na Uvuvi ambazo zinafanya vizuri Mkoani humo.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 11 Agosti, 2023 kwenye mkutano wa wadau na wateja wa Benki hiyo waliotoka kwenye mikoa 8 ya Kanda ya Ziwa ambapo amebainisha kuwa miradi ya zaidi ya Bilioni 285 imewekezwa ambapo kwa zaidi ya asilimia 90 ikiwa ni kwenye Sekta binafsi.
Mhe. Makalla ametumia jukwaa hilo pia kuwapongeza Benki ya maendeleo nchini kwa kuamua kuketi na wateja wake na kuwasikiliza na kupata mrejesho kwani itasaidia taasisi hiyo kuboresha sera zao ili ziendane na wakati lakini pia kubuni huduma na bidhaa mbalimbali kutokana na wakati husika na hali ya ushindani.
"Mkulima mzuri ni yule anayetembelea mashamba yake mara kwa mara, nawapongeza sana TIB kwa uwamuzi wenu wa kukutana na wateja wenu maana nina ushuhuda wa faida za kuwa mteja kwenye benki hii hongereni sana kwani kila mradi mkubwa nchini ukiuliza utaambiwa mwekezaji huyu amewezeshwa na benki ya TIB." Mhe. Makalla.
Amesema Mkoa wa Mwanza unaenda kasi kwenye ukuaji kiuchumi kwani pamoja na uwepo wa fursa za Kutalii, Miradi mbalimbali ya Miundombinu inajengwa kama Bandari, Meli, Daraja la Kigongo-Busisi na Reli ya Kisasa ya SGR hivyo ni wajibu wa taasisi hiyo kushashiwi wadau kuwekeza zaidi kwenye Miradi.
Akigeukia sekta za Uvuvi na Kilimo, Makalla amesema Mkoa wa Mwanza umezungukwa na Ziwa Victoria na ardhi yenye rutuba hivyo wawekezaji wana nafasi ya kuanzisha mashamba ya kisasa na kuanzisha hata kufufua viwanda vilivyosimama ili kuchochea maendeleo.
"Biashara zipo nyingi na mara nyingi kinachotufelisha wateja ni tamaa, naomba niwasihi wateja wa benki ya Maendeleo nchini wekezeni na taasisi hii kwa ufanisi na weledi mkubwa na sio leo unashika hiki unaacha unashika kingine hapo hamtafanikiwa." Amesisitiza wakati akitoa wosia kwa Wateja wa bank hiyo.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo nchini Bi. Lilian Mbassy ametumia wasaa huo kutoa shukrani kwa wateja, wadau wa Maendeleo na watumishi wa taasisi hiyo ambao wamekua sambamba kushirikiana katika kuwainua wafanyabiashara na wadau mbalimbali.
"Lengo kubwa la Mkutano huu ni kuzungumza na wadua wetu, kupata usharuri na kuwasikiliza ni kitu gani wanataka tuboreshe lakini pia ni fursa kwetu kuwapa taarifa ya wapi tunaelekea na huduma gani tumekusudia kuwapatia." Amefafanua Kaimu Mkurugenzi.
Aidha, Mbassy amefafanua kuwa benki hiyo ina mpango mkakati wa miaka 5 wa maendeleo na kwamba wanatoa mikopo ya mitaji ya kuanzia miaka mitatu na vilevile wana huduma ya kutoa ushauri kwa wateja kupitia maandiko mbalimbali ya kibiashara katika kuwasaidia kuwekeza .
Bi. Lilian ameongeza kuwa benki hiyo wanasimamia mifuko maalum hususani miradi ya maendeleo kwa niaba ya wadau na hata kwa niaba ya Serikali katika kuendelea kuleta mageuzi ya kukuza uchumi nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.