RC. MAKALLA AITAKA HALMASHAURI YA SENGEREMA KUKARABATI BOTI YA WAGONJWA
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. CPA. Amos Makalla ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kufanya tathmini ya kukarabati boti ya wagonjwa ambayo ni mali ya Halmashauri inayosafirisha wagonjwa kutoka katika kisiwa cha Juma.
Amesema hayo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa leo Juni 22, 2023 wakati wa Mkutano na Baraza la Madiwani kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za Mwaka 2021/ 2022 katika Wilaya ya Sengerema.
"Hii boti siyo ya muda mrefu sana Halmashauri ikafanye tathmini ya ubovu wa hiyo boti na gharama za utengenezaji na kama gharama za ukarabati ni ndogo kuliko ya kununua mpya basi itengeneze kwa kuwa itawasaidia kuwafikisha kwa haraka wa mama wajawazito na watoto katika vituo vya vya kupatiwa huduma",amesisitiza Mtendaji huyo wa Mkoa
"Hoja hii ya miradi ya zaidi ya Shilingi Milioni 202 ambayo haijakamilika katika ngazi za chini inatakiwa iwe imekamilika ikifika mwisho wa mwezi huu na nitahitaji nipate taarifa ya hii miradi",Balandya
Aidha Ndg. Balandya ametoa rai kwa Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ihakikishe kwamba utaratibu wa ununuzi unazingatiwa kufuatia mapungufu yaliyobainika katika ununuzi na ufungaji wa taa za barabarani katika barabara yenye urefu wa kilomita 5.6 zenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 549.
Pia Ndg. Balandya amemtaka Mganga Mkuu wa wilaya ya sengerema Dkt. Fredrick Mugalura kuhakikisha anafuatilia kibali kutoka TMDA cha kutekeketeza dawa zilizo china zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 42 ili kuepusha athari za matumizi ya dawa hizo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Sengerema Bw. Binuru Shekidele amesema Halmashauri itawaita wananchi waliojenga vibanda vya biashara katika stendi ya Bukala na kuikosesha Halmashauri mapato ya Shilingi Milioni 61.2 ili kuweza kuiona mikataba yao na kufikia makubaliano.
Mwakilishi wa mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali Mkoa wa Mwanza Waziri Shabani amesema kwa hesabu za mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Sengerema ilipata hati inayoridhisha kutoka kwa mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema amesema kwa hoja ambazo zinahusu Halmashauri zifanyiwie mchakato wa haraka wa kuzimaliza ili ziweze kufungwa na kuipatia Halmashauri hati safi ya udhibiti.
Sambamba na hayo Ndg. Balandya amewataka Madiwani wa Wilaya ya Sengerema kuisimamia Halamashauri ili kuhakikisha mapungufu yanarekebishwa na miradi inatekelezwa kikamilifu na kuhakikisha wanawasimamia vijana wanao jiajiri ili kuondoa umasikini katika wilaya hiyo.
Wilaya ya Sengerema Ina jumla ya Kata 26 na Tarafa 3.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.