RC MAKALLA AMEZIAGIZA HALMASHAURI KUPANGA NA KUTOA FEDHA ZA UTEKELEZAJI WA MASUALA YA LISHE KWA WATOTO.
*Ameagiza Wakurugenzi kuwawezesha Maafisa Lishe wa Halmashauri ili watimize majukumu yao*
*Ameziagiza Halmashauri kuweka Agenda ya Lishe kwenye Vikao*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amezipongeza halmashauri za Ilemela, Magu, Kwimba na Jiji la Mwanza kwa kupanga na kutoa fedha kulingana na idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano na amewataka Misungwi, Buchosa na Ukerewe kuhakikisha wanatekeleza Matakwa ya Mkataba wa Lishe ipasavyo.
Ametoa agizo hilo leo Agosti 17,2023 katika kikao cha tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo ameagiza halmashauri hizo kuiga mfano kwa wenzao na kuchukua hatua kabla au ifikapo tarehe 20 Agosti, 2023.
Vilevile, amezitaka halmashauri kuhakikisha wanatoa Elimu ya Lishe kupitia Vikao vyote vya kitendaji ili kila mmoja apate uelewa ili taaluma hiyo isambae na kusaidia kufanikisha adhma ya Serikali ya kuondoa udumavu kwenye jamii.
"Maafisa Lishe wasiwe kimbilio la kazi za dharula hususani kama kupokea wageni wakija kwenye halmashauri, wana majukumu makubwa ya kufuatilia utekelezaji na kutoa Elimu hivyo basi hakikisheni wanapewa usafiri na vitendeo kazi vingine ili wafike malengo." CPA Makalla.
Mhe. Makalla amesema Serikali inaweka msukumo wa kipekee kwenye masuala ya lishe na kwamba Wakuu wa Mikoa wamesaini Mkataba na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu maeneo maalum ya kuwekea mkazo katika Suala la lishe na kwamba Mhe. Rais alitoa viashiria maalum vya kupima utekelezaji wa mkataba huo.
"Lishe duni kwa wanawake wajawazito ni miongoni mwa sababu zinazowaweka katika mazingira hatarishi zaidi yanayoweza kusababisha kujifungua watoto njiti au wafu, watoto wenye utindio wa ubongo au hata mimba kuharibika kabisa." Mkuu wa Mkoa.
Akizungumzia utekelezaji wa maazimio ya kikao cha Mwezi februari mwaka huu kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Claudia Kaluli amesema jumla ya Shilingi Milioni 855.6 zimetumika kwa watoto zaidi ya 846 ambayo ni sawa na Shilingi 1010 kwa kila mtoto ambayo ni sawa na asilimia 110 ya lengo.
Vilevile, Bi Claudia amefafanua kuwa halmashauri za mkoa huo zimeanzisha Klabu za Lishe kwenye Shule za msingi na sekondari kwa asilimia 80% na kwamba kila halmashauri imehakikisha kumekuwepo Madini joto katika chumvi
kutokana na upimaji wa sampuli 4146 uliofanyika.
"Mkoa wetu umepata asilimia 69 kwenye kadi alama ya utekelezaji wa afya za lishe katika kipengele cha Hali ya utoaji wa chakula chenye Lishe kwenye Shule za Msingi na Sekondari katika kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023." Amesema Afisa Lishe Mkoa, Bi. Sofia Lazaro.
Vilevile amefafanua kuwa muongozo unazitaka halmashauri kutoa Shilingi Elfu Moja kwa kila mtoto kuanzia umri wa miaka 0 hadi 5 lakini halmashauri hazijafanya vizuri na kwamba zoezi la utoaji wa chanjo ya matone ya Vitamini A halmashauri zimefanya vizuri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.