RC MAKALLA APONGEZA UBORESHWAJI WA BANDARI NA KUWA MKOMBOZI KUPITIA MRADI WA SGR, MIZIGO MINGI KUFIKA KWA HARAKA MWANZA
*Apongeza mpango wa uboreshwaji Bandari ya Dar utainua uchumi wa Mwanza kupitia mradi wa SGR
*Asema Fela ndiyo kituo Kikuu kitakachokuwa na shughuli nyingi za ushushaji mizigo na abiria,awataka wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi
*Awaondoa shaka wakazi wa kipande cha Fela kuja mjini fidia ya malipo yao kupisha mradi kulipwa mwezi huu
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA. Amos Makalla amepongeza uboreshwaji wa huduma ya Bandari ya Dar kuwa utainua uchumi wa Mkoa wa Mwanza kupitia mradi wa Treni iendayo kasi SGR kutokana na mizigo mingi kufika kwa haraka.
Akizungumza leo eneo la Fela na uongozi wa Kampuni ya CCECC pamoja na uongozi kutoka Wilaya ya Misungwi,.Mkuu huyo wa Mkoa amesema baada ya kupatiwa taarifa ya awali akiwa ofisini kuhusu mradi huo amelazimika kuja kujionea maendeleo yake na amefurahi kazi nzuri ya Mkandarasi huyo.
"Mwanza ni Mkoa uliokaa kimkakati uliopakana na nchi za Maziwa makuu, ujenzi wa reli hii na uboreshwaji wa Bandari yetu hii ina maana wafanyabiashara watanufaika na kufanya shughuli zao kwa uhakika kutokana na mizigo yao kufika kwa usalama na haraka",CPA Makalla
Amewataka wananchi wa Mwanza na hasa wakazi wa Wilaya ya Misungwi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu na mkakati wa kuiboresha Bandari kwani ni faida kwao kiuchumi mara mradi huo wa SGR utakapo kamilika
Aidha amempongeza mkandarasi huyo Kampuni ya CCECC kutoka China kwa kazi nzuri ya kipande cha tano kutoka Isaka kuja Mwanza na ana imani hadi kufika Mei mwakani ujenzi huo utakuwa umekamilika.
"Huu mradi kutoka Isaka hadi Mwanza wa KM 341 umegharimu Shs Trilioni 3 ni fedha nyingi na tunamshukuru Rais wetu kwa ahadi aliyoitoa ya kuiendeleza kikamilifu miradi yote ya kimkakati iliyowachwa na mtangulizi wake wa awamu ya tano Hayati John Magufuli,"amesema CPA Makalla.
"Mhe.Mkuu wa Mkoa mradi wetu wa kipande cha tano kutoka Isaka kuja Mwanza tunaendelea vizuri na tumefikia asilimia 35 hadi sasa, licha ya changamoto ndogo ndogo za kiujenzi kama kuhamisha udongo na kuweka mwingine utakaomudu uzito wa mataluma tunakuahidi hadi kufika Mei mwakani tutakuwa tumeukamilisha," amefafanua Mhandisi Christopher Kalisti,Meneja wa mradi
Akiwa njiani kukagua mradi huo wa SGR Mhe.Makalla amesimama eneo la Mkuyuni Tambukareli na kupata wasaa wa kuzungumza na wananchi ambao wametoa maeneo yao kupisha mradi huo na kuwaondoa shaka kuhusu malipo ya fidia zao ambayo yatafanywa mwezi huu baada ya taratibu zote za msingi kukamilika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.