RC MAKALLA ATEMBELEA MIRADI, AHIMIZA IKAMILIKE KWA WAKATI
*Aitaka Halmshauri ya Jiji kuweka mazingira ya muingiliano wa watu soko la Wafanyabiashara wadogo*
*Awakumbusha kuheshimu taratibu zilizowekwa na Serikali za kutengewa maeneo maalum*
*Stendi kuu ya Mabasi Nyegezi kufunguliwa na Rais Samia*
*Aahidi kusimamia Mradi wa Maji ukamilike kwa wakati wananchi waondokane na kero ya maji*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo Juni 16, 2023 amekagua Miradi ya Soko la Machinga la MchafuKoga, Stendi kuu ya mabasi Nyegezi na mradi wa Maji Butimba Wilayani Nyamagana na kutaka miradi hiyo ikamilike kwa wakati ili kuleta tija ya wananchi.
Akianzia soko la Mchafu Koga linalojengwa kwa gharama ya zaidi ya Shs. bilioni 1.4 ameutaka uongozi wa Jiji la Mwanza kuhakikisha wanafanya shughuli zao katika mazingira rafiki yenye muingiliano wa watu ili wajihakikishie wateja.
"Nimesikia taarifa yenu ya ujenzi wa soko hili, lakini mtambue siyo tu kujenga soko zuri bali mzingatie kufikiwa na wananchi kiurahisi ikiwemo mabasi kupita maeneo haya ili watembea kwa miguu wazione bidhaa kirahisi," CPA Makalla.
Amewakumbusha pia wafanyabiashara hao ndogo ndogo kuendelea kuheshimu taratibu zilizowekwa na Serikali za kutengewa maeneo yao maalum na siyo kukimbilia kupanga bidhaa zao barabarani.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa soko kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Edward Mwamotela amesema ili kuendeleza ujenzi wa Block B na C Halamashauri imepokea Shilingi Bilioni 9 kwa mwaka wa fedha 2022-2023 kutoka mradi wa Green and Smart Cities na kwa mwaka wa fedha ujao 2023-2024 imetengwa bajeti ya shilingi Bilioni 1 kutoka mapato ya ndani.
"Uongozi wa Wilaya na Mkurugenzi kaeni na wadau wote waliopo hapa stendi ili mzisikilize changamoto zilizopo hapa na mzishughulikie na msikilize ushauri wao juu ya namna ya kuendesha standi ili kutoka na mapendekezo mazuri," amesema Mhe. CPA. Makalla.
Amesema wakati Stendi hiyo ya mabasi iliyokamilika kwa asilimia 100 na kuwa katika majaribio kero zote zitatuliwe na atamuomba Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu kuja kuifungua rasmi.
"Ujenzi wa stendi ya Nyegezi umekamilika kwa asilimia 99.5 na kazi zilizobaki ni kufunga Mageti na Stendi imeanza kufanya kazi tarehe 5, Juni 2023, Stendi ya Nyegezi ina eneo la kuegeshea mabasi 120 na magari madogo 80 kwa wakati mmoja,"amesema Edward Mwatomola, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji.
Akikagua mradi wa maji wa Butimba uliogharimu Shs. bilioni 69 na kutarajiwa kuukamilishwa na kukabidhi kwa Serikali Julai 30 mwaka huu na Mkandarasi SOGEA SATTON kutoka Ufaransa, Makalla amesema atausimamia kidete kuhakikisha makubaliano ya makabidhiano yanafanyika kama ilivyopangwa ili wananchi waondokane na tatizo la maji.
Halamashauri ya Jiji la Mwanza ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zinatekeleza miradi ya kimkakati ambayo inalenga kuziwezesha Halmashauri nchini kuongeza mapato na kupunguza utegemezi kwa Serikali kuu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.