RC MAKALLA ATOA SIKU 14 IDARA YA ARDHI KUMALIZA MGOGORO ENEO LA Z.E.K LADHANI
*Awataka watendaji kumpa haki yake mmiliki huyo halali tangia Mwaka 1986*
*Makalla Atinga kwenye eneo husika, athibitisha Maelezo mengi yalikuwa ya uongo*
*Awataka idara ya ardhi Jiji la Mwanza kumpa eneo lake halali au fidia kama wanalihitaji*
*Awataka Jiji hilo kumpa ushirikiano mmiliki na kumwonesha mipaka yake halali*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla amewaagiza Idara ya Ardhi Jiji la Mwanza kumpa haki yake Mmiliki wa Kiwanja namba 1 Kitalu R Mjini Kati ndani ya Siku 14 kwani mgogoro uliopo unatokana na watendaji wa Idara hiyo kutokuwa na weledi.
CPA Makalla amesema hayo mapema leo Novemba 14, 2023 wakati wa kikao chake na kamati ya ardhi ya kushughulikia migogoro uliowakutanisha na wamiliki wa eneo hilo baada ya kufika na kujionea kwa macho uhalisia na kubaini kuwa kuna uzembe upande wa idara hiyo hadi kuibuka kwa mgogoro huo.
Makalla amesema mpango wa maendeleo ya Makazi wa Mwaka 1967 unaonesha wazi kuwa eneo hilo la kiwanja Namba 1, Kitalu R lilimilikishwa kwa Z.E.K Ladhani na si vinginevyo kama anavyosumbuliwa kuendeleza eneo lake kwa sababu zisizo na msingi.
Akitoa majumuisho yake, Mhe. Makalla amewataka Idara ya ardhi kuhakikisha wanamwonesha mipaka yake au wanampa barua ya kumfidia kama Jiji hilo wanalihitaji eneo lake kwa matumizi mengine au wamtake mmiliki wa kiwanja namba mbili wamtake alinunue eneo hilo endapo analihitaji.
Mwakilishi wa upande wa Walalamikaji ametumia wasaa huo Kumshukuru Mkuu wa Mkoa na akatoa pendekezo la kurahisisha mgogoro kuwa TANESCO na TARURA wana nafasi ya kusaidia kwani kuna miundombinu yao kwenye eneo linalolalamikiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.