RC MAKALLA AUKABIDHI RASMI MWENGE WA UHURU SIMIYU,MIRADI YENYE KASORO AHAIDI KUIFANYIA KAZI HARAKA
*Awapongeza wakimbiza Mwenge Kitaifa kwa ukakamavu na uwezo wa kukagua miradi
*Ajivunia ubora wa miradi yenye tija kwa wananchi iliyozinduliwa na Mwenge wa Kitaifa
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe CPA Amos Makalla leo ameukabidhi rasmi Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Simiyu na kujivunia miradi yote iliyozinduliwa na Mwenge huo yenye thamani ya Shs bilioni 21 itakuwa na tija kwa wananchi.
Akimkabidhi Mwenge huo kwenye viwanja vya shule ya msingi Kiloleli Wilayani Busega, kwa mwenzake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt.Yahaya Nawanda,CPA Makalla amebainisha miradi michache iliyobainika na kasoro atahakikisha inafanyiwa kazi na kumpa taarifa kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Abdalla Shaib Kaim kabla ya Julai 31,2023
"Ndugu Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa,miradi ambayo imeonesha utata nakuahidi kutumia vyombo husika kama Takukuru ili kubaini tatizo na hatua za kisheria kuchukuliwa,"amesisitiza Mhe.Makalla.
Ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwenye Wilaya zote 7 zenye jumla ya Halmashauri 8 kwa utulivu na usalama na wanajivunia miradi isiyopungua 50 imeonesha kuwa kwenye ubora na tija kwa wananchi wa Mwanza.
"Asanteni sana ndugu zangu wa Mwanza kwa ukarimu na mapokezi mazuri tangu tulipoingia Mkoani hapa Julai 13,2023,rai yangu kwa viongozi tuendelee kuchapa kazi na kuisimamia vizuri miradi yote inayotekelezwa Mkoani hapa yenye malengo ya kumletea maendeleo mwananchi,tuwe makini kubaini changamoto na kuzipatia ufumbuzi haraka na siyo hadi viongozi wa Kitaifa waingilie kati," amesema Abdallah Shaib Kaim,Kiongozi wa Kitaifa mbio za Mwenge wa Uhuru.
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru inasema "Tunza Mazingira,Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa viumbe hai kwa Ustawi wa Taifa".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.