RC MAKALLA AVALIA NJUGA KILIMO CHA PAMBA KUKUTANA NA MAAFISA UGANI WOTE KUPANGA MKAKATI WENYE TIJA
*Asema Pamba ndiyo zao la kuinua uchumi wa mkulima na Taifa*
*Kukutana na uongozi wa ATCL kuweka mkakati wa ndege ya mizigo iwanufaishe wafanyabiashara*
*Atangaza mpango wa kuinua ufaulu wa wanafunzi na kukomesha utoro shuleni*
*Maafisa ardhi awataka kutokaa ofisini na badala yake kwenda kutatua migigoro ya ardhi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla leo Disemba 8, 2023 amefungua kikao cha bodi ya ushauri wa Mkoa na kuweka bayana mikakati mbalimbali ya kimaendeleo likiwemo usimamizi wenye tija wa zao la Pamba kwa kukutana maafisa Ugani wote hivi karibuni.
Akizungumza na wajumbe wa kikao hicho kwenye ukumbi mkubwa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Makalla amebainisha hakuna sababu ya zao la Pamba kuzorota wakati Serikali imeboresha kwa kiwango kikubwa sekta ya kilimo nchini.
"Wiki ijayo nitakutana na Maafisa Ugani wote kuanzia ngazi ya kata hadi juu, lengo tuone namna ya kulifanya zao hili liwe na tija kiuchumi kwa mkulima na Taifa kwa ujumla" CPA Makalla
Amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwa mkulima kwa kumpunguzia gharama za Pembejeo na kuboresha mbegu bora, hivyo ni wakati mwafaka kwa Mwanza kurudusha uzalishaji na kutoa Pamba itakayokidhi soko la kimataifa.
Kuhusu miradi ya maendeleo ya kimkakati Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi wote kutanguliza maslahi ya Taifa kwa kufanya usimamizi mzuri na hatimaye iwe na tija kwa manufaa ya wananchi.
"Rais wetu ametoa Shs bilioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa ndege,wiki ijayo nikiwa na RAS tutakwenda kuonana na uongozi wa ATCL kwa lengo la ndege mpya ya mizigo iwanufaishe wafanyabiashara wa minofu ya samaki,nyama na mingineyo na hii ni baada ya kuvitembelea viwanda vyao na kusikia kilio chao katika usafirishaji,"amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wakati anazungumza na wajumbe wa bodi ya ushauri wa mkoa
Kwa upande wa migigoro ya ardhi CPA Makalla amebainisha baada ya kuzunguka Wilaya zote za mkoa wa Mwanza amebaini kero nyingi zinatokana na watumishi kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo
"Kuna kiwanja kipo maeneo ya Liberty nimeamuru Halmashauri ya Jiji wamrudishie muhusika halali baada ya kubaini kuwepo na dhuluma ya waziwazi huu ni mfano mmojawapo ambayo ni mbaya kwa watendaji wetu,narudia kusema tukomeshe tatizo hili,"Mkuu wa Mkoa
Aidha CPA Mkalla yupo mbioni pia kukutana na Maafisa elimu wote kuweka kipaumbele cha kiwango cha ufaulu na kukomesha utoro shuleni.
Awali akitoa hotuba fupi,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Mhe.Michael Lushinge amesema kikao cha bodi ya ushauri wa mkoa ndiyo dira ya Mkoa kimaendeleo hivyo kuwataka wajumbe wote kwenda kuifanyia kazi mipango yote itakayowekwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.