RC MAKALLA AWAAGIZA MAAFISA UGANI KUWAFUNDISHA WAKULIMA KANUNI BORA ZA KILIMO
*Awataka kuanzisha mashamba darasa kwenye maeneo yao*
*Awaasa Vijana kujikita kwenye Kilimo na Ufugaji wa Kisasa*
*Awataka vijana kuacha uvuvi haramu na kilimo cha mtandaoni*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ametoa rai kwa Maafisa Ugani wa Kanda ya Ziwa Magharibi kuwatembelea wakulima na wafugaji ili kuwakumbusha juu ya kuzingatia kanuni bora za kilimo na ufugaji ili kuweza kupata tija kubwa kwenye uzalishaji.
CPA Makalla ametoa rai hiyo leo tarehe 8 Agosti 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Kanda ya Ziwa Magharibi katika kilele cha maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yaliyowakutanisha kwa Siku 8 Mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza ambapo ameyafunga rasmi.
"Kwakua ninyi ni wataalamu na ndio kazi yenu msichoke kuwatembelea wakulima na wafugaji na kuwapa ushauri stahiki na katika maeneo yenu ya kazi anzisheni mashamba darasa ili wakulima waendelee kujifunza na kuyaona mafanikio." Amesisitiza.
Aidha, ametoa wito kwa vijana kuacha kufanya kilimo mtandaoni na uvuvi haramu badala yake amewataka kujikita kwenye kilimo na ufugaji wa kisasa wa samaki kwani Rais Samia amekua akitoa fedha nyingi kwenye kuwainua vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ya aina mbalimbali.
"Tafiti mbalimbali juu ya zao la pamba zinaonesha kwenye hekari moja mkulima anaweza kupata kilo 800 hadi 1200 wakati hali halisi ya mavuno kwa mkulima ni kati ya kilo 150 hadi 300 na kwa ng'ombe wa maziwa anaweza kufikia lita 25-30 kwa siku wakati hali halisi kwa sasa lita 10 kwa ng'ombe". Mhe. Makalla.
Vilevile, amebainisha kuwa Mkoa wa Mwanza katika msimu wa 2022/23 ulihekta 455,498.05 na kuzalisha tani 634,373.78 sawa na asilimia 80 hadi kufikia Juni na akabainisha kuwa elimu waliyoipata hapo itawasaidia kufanya mageuzi katika sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Emil Kasagara amefafanua kuwa maonesho hayo yamewapa fursa wadau kutoka sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo huhusisha Utafiti, Umwagiliaji pamoja na hifadhi za Mazao kujifunza kwa vitendo.
"Katika maonesho ya kilimo na sherehe za Wakulima (Nane nane) 2023 jumla ya wadau 863 wameshiriki. Idadi hii inajumuisha Mamlaka za Serikali za Mitaa13, Taasisi za Serikali 11, Taasisi za Fedha 07, Taasisi za Elimu 10, Makampuni ya zana za kilimo 09 pamoja na wajasiriamali wakubwa na wadogo 746." Kasagara.
Maadhimisho hayo ya 2023 yameenda sambamba na kaulimbiu: "Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula."
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.