RC MAKALLA AWAAHIDI USHIRIKIANO WAZEE WA MKOA WA MWANZA
*Asema Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha fedha kuboresha uwanja wa ndege Mwanza, miradi ya maji na miradi ya Kimikakati*
*Awaahidi ushirikiano na watembee kifua mbele wakijivunia uboreshaji wa huduma za kijamii*
*Amesema Serikali itaendelea kushughulikia migogoro ya ardhi kwani imekua ikiathiri kundi hilo*
*Wazee wampongeza kwa kuchapa kazi hasa usikilizaji wa kero za ardhi*
*Amewataka kushirikiana kwa pamoja kukomesha uvuvi haramu ziwa Victoria*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CPA Amos Makalla amesema kuwa Serikali ya Mkoa wa Mwanza itaendelea kuwapa ushirikiano Wazee wa Mkoa huo kwa kuboresha huduma za jamii kwa ajili ya ustawi wao.
Mhe. Makalla ametoa ahadi hiyo leo tarehe 24, 2023 wakati wa kikao chake na wazee hao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ikiwa ni kwa ajili ya kujitambulisha kwao na kusikiliza kero zao na kuzitatua.
Makalla amesema wazee hao ni hazina na Ofisi yake inawaheshimu na kuwathamini sana na kwamba katika kuwatunza kama tunu ya taifa, atahakikisha anakutana na taasisi zote zinazowakwamisha kwenye baadhi ya huduma ili kuziboresha mara moja.
"Mkoa wa Mwanza unawapenda na kuwathamini sana kwani nyie ndio mnaoshauri namna ya kuboresha mambo mbalimbali, tembeeni kifua mbele kwani serikali inawathamini na kuwajali hivyo tutaendelea kuwaboreshea huduma zenu za kijamii." Amefafanua Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa katika kuhakikisha uwanja wa ndege wa Mwanza unakua wa Kimataifa, Serikali inaboresha miundombinu kwa kufanya upanuzi wa eneo la njia ya kutua na kupaa ndege pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa la abiria.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Mkoa amebainisha kuwa yupo kwenye kampeni maalum ya kushughulikia migogoro ya ardhi kwani kundi hilo mara zote wamekua waathirika zaidi hivyo ni lazima limalizwe ili kuwapa amani na ardhi wanazomiliki kwa muda mrefu.
Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Wazee Mkoani humo Charles Masalakulangwa aliwasilisha maombi ya kuboreshewa zao la pamba ili liwe na tija kuanzia upatikanaji wa mbegu bora, kuwezesha maafisa ugani kutoa elimu kwa wakulima na suala la bei yenye tija kwa wakulima ili kuwanufaisha wakulima.
Akitoa taarifa ya Umoja wa Wazee wa Mkoa wa Mwanza (UWAMKOMWA), Mhandisi Greyson Katoya amebainisha matamanio ya wazee kutaka kuboreshewa suala la usafiri wa mjini (Daladala) zisikatishe safari zao ili kuwapa uhakika wananchi wa kufika wanakokwenda na kuondoa changamoto zinazorudisha nyuma zao la pamba.
Mengine ni kuboreshaji wa machinjio ya Nyakato, Mwanza kuwa na soko la Kimataifa la Samaki, kukomeshwa kwa mgao wa maji na uboreshaji wa barabara, kurudishwa hadhi ya zao la pamba, kupatikana kwa mbegu bora za kilimo pamoja na kurejeshwa kwa hadhi ya kituo cha kunenepesha mifugo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.