RC MAKALLA AWAALIKA WAWEKEZAJI KUTUMIA FURSA YA RELI YA KISASA KUJENGA BANDARI KAVU MWANZA
*Asema reli hiyo itafungua usafirishaji wa mizigo nchi za Maziwa Makuu*
*Asema kipande cha Mwanza- Isaka chafika asilimia 35% ya ujenzi*
*Awapongeza Shirika la Reli kwa uzinduzi wa kipande cha Dsm -Morogoro*
*Asema Daraja la Kigongo-Busisi lafikia asilimia 85 ya ujenzi*
*Mwanza kuzindua mpango mkakati wa utalii*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewaalika Wawekezaji kutumia fursa ya uwepo wa Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR) kuwekeza kwenye ujenzi wa Bandari Kavu Mkoani humo hususani eneo la Stesheni ya Fela wilayani Misungwi.
CPA Makalla amesema hayo leo tarehe 05 Machi 2024 wakati akitoa salamu za Mkoa huo kwenye ufunguzi wa Kongamano la siku mbili la uwekezaji katika Sekta ya Reli linalofanyika kwenye Hoteli ya Malaika Mkoani Mwanza.
Amesema, ukamilifu wa Bandari hiyo utafanya kuwe na ongezeko kubwa la shehena ya mizigo mkoani humo itakayosafirishwa kutoka bandari ya Dar es salaam hivyo eneo la uhifadhi wa mizigo litakua kwenye uhitaji mkubwa.
"Tumeona bandari ya Dar es salaam inaboreshwa, sasa mizigo itashushwa kwa kiwango kikubwa pale na kusafirishwa kupitia reli yetu ya kisasa ambapo Mwanza tumebahatika kwani ndio mwisho wa reli hii sasa ni lazima tujipange kuchangamkia fursa hiyo." Makalla.
Aidha, amelipongeza shirika la Reli nchini kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa reli ya kisasa hususani kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro ambacho kimeshakamilika na kuzinduliwa huku akibainisha maendeleo mazuri ya ujenzi wa kipande cha Isaka -Mwanza.
"Kama mizigo hii yote itakuja Mwanza, je sisi tutapakia nini kwenye treni yetu kurudi kwenye bandari ya Dar es salaam, tumejipanga kuhamasisha kilimo chenye tija Mwanza, ufugaji wa kisasa na usindikaji wa samaki na madini ili tuingie kwenye mzunguko wa kibiashara" amesisitiza Makalla.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Kigongo-Bisisi uliofikia zaidi ya asilimia 85, Makalla amesema Mkoa huo unaandaa mpango mkakati wa kuchochea Utalii kwani hata uwanja wa Ndege unapanuliwa na kuboreshwa kuwa wa Kimataifa na kwamba jengo la kisasa la abiria linaanza kujengwa.
Mhe. David Kihenzile, Naibu Waziri Wizara ya Uchukuzi amebainisha kuwa utekelezaji wa Reli ya kisasa inayotumia umeme imeiweka Tanzania kwenye viwango vya kimataifa vya usafirishaji kwa kutumia Reli ya kisasa inayotumia umeme na kuhifadhi mazingira.
"Hili si jambo la kawaida (ujenzi wa Reli ya kisasa) si jambo la kawaida, vipande vyote 7 vimeanza kwenye maono na baadae kupata fedha jambo ambalo nchi nyingi zimeshindwa kutekeleza hata kwa kukopa lakini sisi tunaweza, mambo haya ni yakujivunia." Mhe. Kihenzile.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli nchini Masanja Kadogosa amesema Serikali imejipanga kujenga zaidi ya Kilomita 4700 za Reli ya kisasa ili kumtia moyo Rais Samia mwenye ndoto ya kuhakikisha kwamba fursa ya kuwa na mazingira bora kijografia kwa nchi za Afrika Mashariki.
"Biashara haiwezekani bila kuingiliana, Afrika tunaunganishwa na Reli, Ndege, Meli hivyo sisi (Tanzania) ni lazima tuone tunaboresha miundombinu yetu ya kiuchukuzi ili kwenda sambamba na fura hizo" Mkurugenzi Mtandaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.