RC MAKALLA AWAHAKIKISHIA USHIRIKIANO WAANDISHI WA HABARI MWANZA
*Amewashukuru Waandishi kwa kutumia vema kalamu zao kuunganisha jamii*
*Aelekeza Taasisi zote Mwanza kutoa ushirikiano kwa wanahabari*
*Awaasa wanahabari kuandika kutoka kwenye vyanzo vya uhakika na ukweli*
*Abainisha ujenzi wa Jengo la Abiria la kisasa Airport Mwanza kuwa Kimataifa*
*Aahidi usaidizi wa Pikipiki 2 na kuongoza Harambee ya ujenzi wa ofisi*
*Awasihi kutangaza miradi ya kimkakati na timu za Mwanza kucheza Ligi kuu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amesema Ofisi yake itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari kwenye kuhabarisha umma na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kwa wakati na kwa uhakika.
Makalla amesema hayo leo Februari 23, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa huo kupitia chama chao (MPC) katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Makalla ametumia wasaa huo kubainisha furaha yake kwa waandishi wa habari hao kwani wamekua kiungo cha kuwafikia wananchi na ameomba umoja udumishwe zaidi kwenye ofisi mbalimbali ili kuifanya Mwanza kukua zaidi kiuchumi na maendeleo ya huduma za Jamii.
Aidha, amebainisha mpango wa Serikali wa kuboresha uwanja wa Ndege wa Mwanza kuwa wa Kimataifa hususani ujenzi wa Jengo la abiria la kisasa litakaloanza kujengwa ndani ya wiki mbili zijazo na kwamba utasaidia kukuza utalii mkoani humo.
Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko ametumia wasaa huo kuwasilisha ombi kwa Mkuu wa Mkoa kuwa mgeni rasmi kwenye Harambee ya Kuchangia fedha za ujenzi wa Ofisi ya Chama hicho itakayofanyika siku za usoni.
Aidha, Soko amebainisha kuwa waandishi wa habari mkoani humo wapo kwa ajili ya kuhabarisha umma na kusaidia kupatikana kwa majawabu ya changamoto mbalimbi kwa jamii jambo ambalo wanafanya kwa weledi na kuzingatia maadili ya uandishi.
"Tunafanya kazi zetu kwa kuzingatia weledi na maadili hususani kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025" Amesema Mwenyekiti Soko.
Vilevile, ametumia wasaa huo kuziomba taasisi na mamlaka zote za Serikali Mkoani humo kuhakikisha wanazingatia usalama wa waandishi wa habari wakati wote wanapotumikia shughuli za uhabarishaji wa umma na kutowazungusha waandishi mara wanapohitaji taarifa.
Katika kuhakikisha wanakua na Ofisi yao na kuondokana na gharama za kupanga, Soko ametoa rai kwa Mkuu wa Mkoa kuwasaidia waandishi wa Habari kwenye upatikanaji wa vitendea kazi mbalimbali vya Studio na vinginevyo pale ambapo Makalla ameridhia na kuahidi kuwanunulia Pikipiki 2 siku za usoni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.