RC MAKALLA AWATAKA MWATEX KUWA WABUNIFU KUKABILI USHINDANI SOKO LA NGUO
*Awataka kuendana na soko la kisasa kwa kuwa wabunifu na wenye mikakati dhahiri ya kuinuka kibiashara*
*Awaagiza TANESCO na MWAUWASA kuwa na ratiba ya huduma inayofahamika kwa wateja*
*Atoa rai kwa kitengo cha biashara kutangaza kiwanda hicho ili kupata malighafi*
*Awaahidi kushirikiana nao kuboresha huduma katika kuendelea kufanya uzalishaji*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wamiliki wa kiwanda cha uzalishaji nguo MWATEX 2001 LTD kuzalisha bidhaa nzuri na bora zinazokidhi soko la sasa kwenye jamii ili kujihakikishia katika eneo hilo
Mhe. Makalla ametoa wito huo mapema leo Disemba 05, 2023 alipofanya ziara kwenye kiwanda hicho kilichopo Nyakato na kubaini kushuka kwenye uzalishaji hadi Mita laki 5 kutoka Milioni 1 kwa mwaka pamoja na uwepo wa malighafi hususani pamba mkoani humo.
Amesema, pamoja na changamoto zingine ni lazima kiwanda hicho kiwe na mkakati wa mipango ya muda mfupi na mrefu katika kuzalisha bidhaa bora na kuhakikisha wanayafikia malengo waliyoyapanga ya uzalishaji aidha wa kanga, shuka, mifuko na vitenge.
"Lengo la Serikali kubinafsisha viwanda hivi ni kupata tija hivyo ni lazima muongeze ubunifu ili kuyafikia malengo ya Serikali ya kuona vinazalisha na siyo kujificha kwenye visingizio mbalimbali" Mkuu wa Mkoa.
Vilevile, ametoa rai kwa kiwanda hicho kuboresha kitengo cha biashara ili kutangaza bidhaa zao huku Serikali ikiendelea kushirikiana nao kwenye kuboresha huduma za nishati ya maji na umeme.
Aidha, amewataka TANESCO na MWAUWASA kuwa na ratiba inayofahamika ya mgao wa huduma zao ili wenye viwanda waweze kujipanga kwenye uzalishaji kwani wanapokata bila taarifa wanawasababishia kupata hasara.
Katika kufafanua suala la nishati ya Umeme, Meneja wa TANESCO Kanda ya Nyakato Mhandisi Jackson Peter amesema matatizo ya kukatika kwa umeme yanakwenda kuisha siku za usoni lakini wataboresha utoaji wa taarifa kwa wakati.
Awali Bi. Mariam Msangi, Afisa Masoko wa kiwanda hicho alibainisha changamoto kadhaa zikiwarudisha nyuma kama uwepo wa nguo za mitumba na jamii kuacha kutumia mavazi ya asili, kukatika kwa maji na umeme pamoja na bei kubwa wanazotozwa na watoa huduma hizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.