RC MAKALLA AWATAKA WAKUU WA WILAYA KUSIKILIZA KERO ZA WAFANYABIASHARA KABLA YA MWEZI DISEMBA KUISHA
*Awaagiza Wakuu wa Wilaya kukutana na wafanyabiashara ndani ya mwezi Disemba kutatua kero zao*
*Awaagiza LATRA kuacha uzembe na kusimamia sheria za usafirishaji na siyo kupindisha*
*Awataka watendaji wa Serikali kubadilika, aagiza kuwahudumia wafanyabiashara kwa weledi*
*Awaagiza Halmashauri ya Jiji kummilikisha Z.E.K Landan kiwanja namba 1, Kitalu R mjini kati mara moja*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka Wakuu wa wilaya mkoani humo kufanya mikutano ya kusikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara kabla ya kuisha kwa mwezi Disemba mwaka huu ili kwa pamoja waweke uelewa wa pamoja wa namna ya kuboresha biashara zao.
Makalla ametoa agizo hilo leo Disemba 06, 2023 wakati akihitimisha kikao na Jumuiya za wafanyabiashara mkoani humo aliokutana nao kwa zaidi ya saa 5 kwenye ukumbi wa Mikutano mkoani hapo kuwasikiliza na kutatua kero zao ikiwa ni katika kuhakikisha wanaboresha biashara kwa pamoja.
Aidha, amewataka watendaji kila sekta kwenda kuangalia namna gani tozo zilizopo zinawaminya wafabyabiashara badala ya kuwainua zikiwa pia ushuru wa huduma ili kutoka na pendekezo la namna ya kuboresha na kuondoa sintofahamu hizo hususani utitiri wa tozo huku zingine zikionekana kujirudia baina ya taasisi.
"Watendaji wa mamlaka ya mapato na na maafisa biashara tuwe na lugha nzuri ya kudai kodi na kuwatia moyo watu ili wafanye biashara maana Serikali inaweka mipango mbalimbali ya kuboresha huduma za jamii kwa kutumia kodi hivyo ni lazima tutengeneze mahusiano mazuri na wafanya biashara na sio kuwakatisha tamaa."
Katika kushughulikia adhabu za makosa ya maegesho, Mkuu wa Mkoa ameagiza kuwekwa kwa vibao kuonesha sehemu zinazoruhusiwa na kukatazwa kwa wenye usafiri kuegesha badala ya kusubiri watumiaji wa barabara wafanye makosa ili wawatoze faini na pia akaagiza Jiji la Mwanza kumpatia haki yake Z.E.K Landan kwa kumnilikisha eneo lake lililopo mjini kati.
"Huu ni uzembe ni tabia ya watu kupindisha sheria, nataka operesheni ya kusimamia hatua hiyo ili daladala, bodaboda na bajaji zifuate taratibu zilizowekwa nawaagiza wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na LATRA kwenda kushirikiana kuondoa changamoto" Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, Mwenyekiti wa chemba hiyo Gabriel Chacha ametumia jukwaa hilo kuwasilisha kero 20 zinazowakabili huku zikijikita zaidi kwenye masuala ya utitiri wa Kodi, tozo, ushuru na leseni kinzani kwenye utoaji wa huduma na mamlaka za Serikali kuingiliana kwenye utozaji kwenye mambo yanayofanana.
"Sasa hivi kila mmoja ahakikishe anakwenda kwenye chuo cha mafunzo ya udereva asome apate cheti ndipo awe na sifa za kuwa na leseni na kuingia barabarani kuendesha gari, hii itasusaidia sana kuwa na usalama kuliko hali ilivyo sasa watu wana vyeti vya udereva bandia" Amesema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa.
Mrakibu wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, SF Labani Kamila ametumia wasaa huo kuwataka wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo wanapokua na mipango ya ukaguzi wa stoo zao za bidhaa ili wawashauri namna nzuri ya kupanga ili kuepuka athari za moto na kuwa na vifaa vya kuzimia moto vinavyobebeka.
Naye Stella Marwa, Meneja Shirika la Bima la Taifa (NIC) kanda ya ziwa ametoa wito kwa wafanyabiashara kujisajili kwenye bima ili kujihakikishia ulinzi wa biashara zao wakati wa maafa kama moto kwani bima ipo kwa ajili ya kuwafanya wasipate hasara na sio kuwatia hasara.
Wakati huohuo, Meneja wa Uwanja wa ndege wa Mwanza Mussa Mcholla amewasihi wafanyabiashara kutumia uwanja huo kusafirisha mizigo kwenda nchi mbalimbali duniani zikiwemo China na zote barani Afrika kwa kutumia shirika la ndege kwani Rais Samia amenunua ndege kubwa yenye tani 54.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.