RC MAKALLA AWATAKA WANACHAMA WA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA NYANZA KUWA WAZALENDO NA KUJENGA USHIRIKA IMARA
*Abainisha kurejeshwa kwa Akaunti Maalum (ESROW ACCOUNT) ya Chama Kikuu cha Ushirika NYANZA*
*Ataka kutumika vizuri kwa Akaunti hiyo katika kufufua Ushirika na kuleta tija*
*Ataka Chama kujipanga kushindana katika Soko na sio kukopa Wakulima*
*Awataka kuwa na mkakati wa kufufua viwanda vya kuchaka pamba*
*Awataka kusimamia upatikanaji na ugawaji wa pembejeo za Kilimo kwa wakati*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka Chama kikuu cha Ushirika Nyanza kulinda Mali kwa uzalendo na kuwa na hatimiliki ili zisipotee badala yake ziendelezwe ili zizalishe Mapato na kuwa na Chama imara chenye Ushindani sokoni.
Mhe. Makalla ametoa neno hilo mapema leo Machi 27, 2024 wakati akifungua Kikao cha Siku moja cha Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU- Nyanza Cooperative Union) kilichofanyika kwenye chuo cha Ualimu Butimba.
Amesema, katika kuimarisha Ushirika ni lazima kila mmoja kwenye umoja huo awe mzalendo katika kulinda mali na vitega uchumi za chama hicho kama Mashamba, Magari, Maghala, Nyumba, Viwanda n.k ili visaidie kukuza ushindani na kupanua biashara ili zisaidie kukuza uchumi wa chama hicho.
Aidha, amewataka kuhakikisha wanaboresha mnyororo wa thamani wa zao la Pamba kwa kufufua viwanda vya kuchambua pamba kwani kwa kufanya hivyo wataongeza thamani ya zao hilo, uhakika wa soko na kipato kwa wanachama wake na sio kukopa mazao kwa wakulima na baadae kutafuta masoko.
Vilevile, amewataka wanaushirika kusimamia upatikanaji na ugawaji wa pembejeo za Kilimo cha Pamba kwa wakati kwa wanachama wake, pia akawaagiza Maafisa Ugani kujiridhisha na takwimu za Mahitaji ya Pembejeo za wakulima wa pamba ili kuwezesha kuwa na takwimu sahihi za mahitaji ya pembejeo hizo kwa wakulima.
"Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) imeanza kutumia mfumo wa TEHAMA, tunataka kuhakikisha wanachama wote wanajisajiri kwa 100% na kuzingatia matumizi ya miongozo 15 ya biashara ili kuendana kiushindani." Amesema Gabriel Mwita, Mwakilishi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini.
Vilevile, Mwakilishi huyo wa Mrajis amezungumzia uwekezaji unaotarajiwa kuanza rasmi mwezi Mei mwaka huu ambao utawafanya washirika kuwa na asilimia 51 za hisa ili waweze kuimiliki benki ya Ushirika na kwamba kwenye vyama vya ushirika kunakua na SACCOS ili kuinua mitaji ya wanachama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.