RC MAKALLA AWATAKA WATENDAJI WA KATA KUTENGA SIKU MOJA NDANI YA WIKI KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI
*Awataka kuwajibikwa kwa wananchi kwani ndio Dira ya Rais Samia*
*Aziagiza taasisi za umma kutekeleza maagizo anayoyatoa kwenye Mikutano ndani ya siku 14*
*Aagiza Halmashauri kushirikiana na Wizara ya Ardhi kumaliza Mgogoro wa ardhi kwenye kijiji cha Nyambitilwa*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe CPA Amos Makalla amewataka Watendaji wa Kata kutenga siku maalum ndani ya juma mayhalani Alhamisi kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kuwasilisha muhtasari wa zoezi hilo kwa Mkurugenzi wa Mtendaji mara moja.
Ametoa agizo hilo leo Oktoba 19, 2023 wilayani Magu akiwa kwenye Mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi ambapo amebaini msingi wa migogoro na kero nyingi unatokana na kulimbikizwa kwa dukuduku kwa wananchi kukosa msaada wanapohitaji kutoka kwa watendaji hao.
Aidha, CPA Makalla amesema amegundua kuwa uwajibikaji wa watendaji wa vijiji na kata umekua wa kusuasua na ndio maana hata kwenye mikutano yake ya kusikiliza kero mahudhurio ya wataalam hao yamekua hafifu hususani Magu ambapo alipokua akianza usikilizaji wa kero kulikua na watendaji 10 tu Kati ya 25 waliopaswa kuwepo.
"Nataka watendaji muwajibike sikubaliani na hali ya kuchukulia mzaha kwenye mambo ya msingi, hapa mlipaswa muwepo watendaji 25 lakini ni kumi tu ndio wamefika hapa maana yake hawataki kufahamu matatizo ya wananchi wao na ndio tunaona migogoro inazidi kuongezeka kila siku wataki walipaswa kuimaliza huko." Mkuu wa Mkoa.
Vilevile, amewataka watendaji wa Halmashauri na Taasisi zingine kukamilisha utekelezaji wa Maagizo na maelekezo anayoyatoa kwenye mikutano ya kusikiliza kero ndani ya siku 14 ili kutoa majibu ya kila suala lililoibuliwa na kuhitaji ufuatiliaji au utekelezaji kwa kutumia nyaraka au vielelezo mbalimbali.
"Watendaji naendelea kuwataka mtoke maofisini mkasikilize na kuhudumia wananchi, mtumie lugha ya staha yenye kujenga matumaini ili kujenga imani na uaminifu kwa wananchi ambao Rais Samia amejipambanua kuwa yupo kwa ajili ya kuwaboreshea huduma." Amesema.
Katika kutatua kero iliyowasilishwa na Ndg. Renatus Madoshi ya wananchi kutakiwa kulipa kodi ya ardhi kwenye kijiji cha Nyambitilwa ambapo mwaka 2009 halmashauri ililitwaa eneo lao (Mashamba) na kurasimisha na baadae kushindwa kulipa fidia na 2020 kuamua kulirudisha kwa wananchi ,Mhe. Makalla ameiagiza halmashauri kuwasilisha kero hiyo kwa Waziri wa Ardhi kwa ajili ya utatuzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.