RC MAKALLA AWATAKA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA BIDII ILI KULILETEA TAIFA MAENDELEO
*Awaasa watumishi kuwa na weledi, bidii na wazalendo kwa Taifa*
*Ataka taarifa ya utekelezaji wa shughuli kutolewa katika kila robo*
*Baraza laipongeza Idara ya Utumishi RS Mwanza kwa kujali watumishi*
Mhe. Amina Makilagi, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana amewataka Watumishi na waajiri Mkoani Mwanza kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kuwahi kazini, kutunza mali za umma na kuwa wazalendo ili kukuza utumishi kwa pamoja na kuliletea Taifa maendeleo.
Mhe. Makilagi amesema hayo leo Machi 16, 2024 wakati akilihutubia Baraza la wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza lililofanyika kwenye Ukumbi wa Wag Hill Resort chini ya Kaulimbiu ya 'Tutatue Changamoto kwa Pamoja'.
Aidha, Mhe. Makilagi amesema mpango wa bajeti katika idara ni lazima uwe shirikishi kwa watumishi ili kila mmoja ajue ni shughuli gani itatekelezwa na kwa wakati gani, na sambamba na hilo akatoa wito kwa watumishi kutofuja fedha za umma na kuepuka rushwa mahala pa kazi.
Mwenyekiti wa baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza Emily Kasagara ametoa wito kwa watumishi kushirikiana katika kutimiza Dira ya maendeleo ya miaka mitano na kufanya kazi kwa bidii, weledi, juhudi na kuwa wabunifu ili kujenga Taifa uchumi wa nchi.
"Hadi kufikia mwisho wa mwaka mwezi Juni, 2023 jumla ya Sh. 478,226, 133,790 zilipokelewa sawa na asilimia 96.6 ya fedha zote zilizoidhinishwa na kwamba hiyo ni sawa na asilimia 95 ya fedha zilizopokelewa," amefafanua Mkuu wa Seksheni ya Mipango na Uratibu Henry Mwaijega.
Mwaijega ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24 Mkoa umeidhinishiwa kutumia zaidi ya Bilioni 487 na kwamba kumekua na ongezeko la Bilioni 16.8 sawa na asilimia 3.5 ikilinganishwa na 2022/23 huku ongezeko hilo likitokana na fedha za mishahara, matumizi mengineyo na fedha za miradi kutoka serikali kuu kuongezeka.
Halikadhalika, amewasilisha pia rasimu ya Bajeti ya Mkoa na Halmashauri zake kwa mwaka 2024/25 inayoonesha kuwa mkoa umepanga jumla ya Sh. 523, 067,403,641 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. zikijumuisha zaidi ya Bilioni 308 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Bilioni 142.5 kwa shughuli za maendeleo.
Akiwasilisha taarifa za kiutawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu Bi. Franciscar Mmari amesema hadi kufikia Disemba 2023 watumishi 25 wa kada mbalimbali walipandishwa vyeo huku 5 hawakupandishwa kutokana na kukosa sifa za muundo kwa mujibu wa miundo ya maendeleo ya utumishi wa kada zao.
Aidha, ametoa rai katika uandaaji wa ikama na bajeti ya mishahara uzingatie miundo ya maendeleo ya utumishi, miundo ya mshahara, mfumo wa usimamizi wa taarifa za kiutumishi na mishahara pamoja na bajeti kutengwa na kituo cha kazi husika na si vinginevyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.