RC MAKALLA AZINDUA JENGO LA WAGONJWA WANAOHITAJI UANGALIZI MAALUM (ICU) BWISYA-UKARA
*Lajengwa kwenye Hospitali yenye hadhi ya Wilaya Bwisya -Kisiwani Ukara*
*Awapongeza wasimamizi kwa kuokoa fedha zaidi ya Milioni 70 zilizojenga nyumba ya watumishi*
*Aagiza Ofisi ya Mganga Mkuu Mkoa kupanga ratiba za Madaktari bingwa kufika kwenye hospitali hiyo*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla, leo Novemba 22, 2023 amezindua jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum lililojengwa kwenye Hospitali ya Bwisya kwenye kisiwa cha Ukara kwa Shilingi Milioni 177 kati ya 250 zilizotengwa.
Akiongea na watumishi na wananchi, CPA Makalla ameipongeza halmashauri ya Ukerewe kwa usimamizi mzuri wa mradi uliopelekea kuokoa fedha zaidi ya Milioni 70 ambazo zimesaidia kujenga nyumba ya watumishi ya familia tatu kwenye hospitali hiyo baada ya kuongeza milioni 30 kutoka kwenye mapato ya ndani.
Mhe. Makalla amesema Rais Samia amewaletea huduma hiyo karibu kwa upendo wake kwani awali wananchi waliokua wakihitaji huduma hizo walilazimika kusafiri kwenda kwenye kisiwa cha Nansio wilayani Ukerewe jambo ambalo lilihatarisha afya zao.
"Nimezunguka ndani ya jengo hili (ICU) na nimeona limejengwa katika viwango bora na limewekewa vifaa vya kisasa kwa mahitaji ya kutibu wagonjwa watakaokua kwenye hali mahututi hivyo naomba mvitunze na kero ya watumishi wachache ninakwenda kulifuatilia", amesema Makalla.
Halikadhalika, ametumia hafla hiyo kumuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kupanga ratiba za Madaktari bingwa kutoka kwenye hospitali ya rufaa ya Kanda Bugando kufika kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa kwani jiografia inawapa ugumu kuzifuata jijini Mwanza.
"Uchache wenu (watumishi) usiwapelekee mkatoa huduma hafifu, tuendelee kuhudumia wananchi kwa upendo nami kwa nafasi yangu nitafuatilia suala la watumishi kuletwa hapa." Amesema Mhe. Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kwa niaba ya wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.