RC MAKALLA AZINDUA RASMI USIKILIZAJI WA KERO ZA WANANCHI MWANZA
*Aagiza kwa wakuu wa Wilaya kila siku ya alhamisi iwe ya kusikiliza kero za wananchi
*Atoa agizo kwa Maafisa kutoa ushauri wa kisheria mapema kwa wananchi kabla ya shauri kufikishwa Mahakamani*
*Awataka watumishi kuwa na uwajibikaji wenye tija wa kusikiliza na kutoa maamuzi kero za wananchi
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA. Amos Makalla leo Septemba 18, 2023 amezindua rasmi zoezi la kusikiliza kero za wananchi Mkoani humo na ametoa maagizo kwa wakuu wa Wilaya kila siku ya alhamisi iwe ya kusikiliza kero za wananchi kwa kuwasikiliza na kutoa maamuzi
Akizindua kampeni hiyo kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa akiambatama na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali CPA Makalla amebainisha utaratibu huo ulkifanyika kikamilifu utaondoa kero nyingi za wananchi na kutowafikia viongozi wa juu wanapokuja kuwatembelea maeneo yao.
"Nimeunda kikosi kazi cha kuzungukia Wilaya zote kupokea taarifa za migogoro ya ardhi lakini niwahimize maafisa ardhi toeni mapema ushauri wa kisheria kwa wananchi hali itakayowasaidia kupata haki zao mapema," amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Ameongeza kuwa kumekuwa na kero kubwa kwa wananchi hasa eneo la ardhi ambapo idadi kubwa wamekuwa wakipoteza haki zao kutoka kwa baadhi ya watu wenye uwezo ambao wamekuwa wakikimbilia mahakamani na kushinda mashauri husika kutokana na wananchi kushindwa kupata tafsiri vizuri za kisheria na kujikuta wakipoteza haki zao.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa ufafanuzi usikilizaji wa kero hizo siyo kwa mashauri ambayo tayari yametinga mahakamani kwani kisheria hana mamlaka ya kuingilia mhimili huo,hivyo amewataka wananchi kuwasilisha matatizo yao ambayo hayajafika kwenye vyombo vya sheria.
"Leo nafanya uzinduzi huu nikiamini mmepata somo la kujifunza namna ya kushughulikia kero za wananchi, sitarajii nikifika kwenye Halmashauri zenu nikute idadi kubwa ya wananchi wenye kero na badala yake mkafanye kazi hii kwa umakini na utatuzi haraka",amesisitiza CPA Makalla kwa viongozi.
Katika uzinduzi huo wa kusikiliza kero za wananchi kutoka Wilaya za Nyamagana na Ilemela,wananchi wengi waliojitokeza walikuwa na kero za ardhi ambazo baadhi mashauri tayari yalikuwa mahakamani na kero zingine Mkuu huyo alizipatia ufumbuzi hapo hapo.
Baada ya uzinduzi huo Wakuu wa Wilaya wote kutoka Mkoani Mwanza wataendelea na zoezi hilo kwenye vituo vyao kwa kujipangia utaratibu wa siku za kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi kuanzia kwenye ngazi za vitongoji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.