RC MAKALLA AZITAKA HALMASHAURI KUKAMILISHA MIUNDOMBINU YA MADARASA ILI KUPOKEA WANAFUNZI 2024
*Amezitaka Halmashauri kukamilisha ujenzi madarasa ya awali, Msingi na Sekondari*
*Aagiza kamati za isalama na watendaji kushirikiana kukomesha utoro na watoto kuanza shule mara moja*
*Awataka waratibu elimu wa kata kusimamia kuboresha ubora wa elimu*
*Awapongeza walimu na viongozi wote kwa kupandisha ufaulu darasa la saba*
*Awataka viongozi kuhamasisha wazazi ili kuwa na programu ya chakula kwa wanafunzi shuleni*
*Awataka watendaji kutumia taasisi za elimu kupata maoni ya uboreshaji wa sekta*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka viongozi kwenye wilaya zote mkoani humo kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo hadi kufikia mwanzo wa muhula mpya wa masomo mwezi januari 2024 ili kuwa tayari kupokea wanafunzi.
CPA Makalla amesema hayo mapema leo Jumanne ya 19 Disemba, 2023 wakati wa kikao kazi cha wadau wa elimu kilichokutana mahsusi kuweka mikakati ya kupokea watoto wanaojiunga na shule za awali, msingi na sekondari ndani ya Mkoa wa Mwanza hususani ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya madarasa.
Amesema halmashauri zinapaswa kukamilisha miundombinu ya madarasa ipasavyo kama Serikali ilivyoagiza ili kutoa nafasi kwa watoto waliofikia umri wa kujiunga na shule za awali na waliofaulu kwenda sekondari waweze kujiunga mara moja na kwenye hilo kamati za usalama na watendaji lazima washirikiane pamoja na kukomesha utoro kwa wanafunzi.
"Sitarajii kusikia mtumishi au kiongozi wa Sengerema anakula sikukuu sehemu fulani ndani ya huu muda wakati mpo asilimia 45 tu ya utekelezaji wa agizo la kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya elimu, fanyeni kazi usiku na mchana harakisheni kazi hii ili mtoke mlipo na ifikapo mwanzo wa muhula muweze kupokea watoto." Mkuu wa Mkoa.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza Martine Nkwabi amefafanua kuwa jumla ya shule za Msingi 991 za Mkoa huo zilifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2023 kwa watahiniwa 92, 655 ambapo watahiniwa 78, 437 ikiwa ni asilimia 84.7 (wavulana 36,397 na wasichana 42,040) wamefaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2024.
"Matokeo yameonesha asilimia ya ufaulu wa Mkoa imepanda kutoka asilimia 82.63 ya mwaka 2022 hadi 84.72 sawa na ongezeko la asilimia 2.09 na ongezeko hilo limetokana na Halmashauri zote 7 kupandisha ufaulu ikiongozwa na Halmazhauri ya Misungwi iliyopanda kwa asilimia 5 japokua ni ya mwisho kimkoa kwa ufaulu" Amesema Afisa Elimu.
Ameongeza kuwa pamoja na uwepo wa miundombinu na vifaa bora shuleni bado watendaji wa kata, vijiji na mitaa wana nafasi ya kuhamasisha wazazi kupeleka watoto shule na kuona namna ya kusaidia kuwepo kwa programu ya chakula shuleni ili kuthibiti utoro shuleni na kwenye suala hilo ameitaja Mwanza kuwa nafasi ya 21 kama Mkoa kutoa chakula shuleni.
Awali, Afisa Elimu awali na msingi Jiji la Mwanza, Mwalimu Musa Langwe akijibu tuhuma za Halmashauri hiyo kuwa na msongamano wa wanafunzi amebainisha kuwa shule ya Nyerere na zingine ndani ya Halmashauri hiyo wana upungufu wa zaidi ya madarasa elfu 1 lakini wanaendelea na ujenzi wa madarasa 3 kwenye shule hiyo na zingine ili kukabiliana na tatizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.