RC MAKALLA HAJARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI KISIWANI KOME, ATAKA UKAMILISHWE HARAKA
*Amtaka Mkandarasi kuweka mkakati wa ukamilishaji mara moja*
*Asema ni uzembe kutokamilisha mradi huo tangu Agosti, 2023*
*Ataka nguvu zaidi kuwekwa kwenye ujenzi wa chanzo cha mradi huo*
*Aagiza kuwekwa mpango wa chakula shuleni ili kuwa na mahudhurio bora*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amemtaka Mkandarasi Kamba's Group of Companies Ltd anayejenga mradi wa maji wa Bugoro- Lugata kwenye Kisiwa cha Kome kukamilisha mradi huo ifikapo Mwishoni mwa mwezi februari mwaka huu.
CPA Makalla ametoa agizo hilo mapema leo Januari 16, 2024 akiwa ziarani kisiwani humo baada ya kukagua mradi huo unaotekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 2.2 na kubaini uzembe kwenye utekelezaji uliopelekea kutokamilika kwa mujibu wa mkataba tokea mwezi Agosti 2024 huku msimamizi na Mkandarasi wakigubikwa na visingizio.
"Nataka niwaambie nyie (RUWASA), mkiendelea kucheka na wakandarasi wa namna hii mtatukwamisha, nataka ndani ya wiki moja Meneja RUWASA wa Wilaya unipe taarifa ya mpango wa kukamilisha mradi huu ifikapo mwezi ujao mwishoni, nataka Meneja na Mkandarasi mtimize wajibu wenu kuanzia sasa." Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa amesema kupitia mpango wa maendeleo ya maji (WSP) chini ya Programu ya usambazaji Maji vijijini na Usafi wa Mazingira (RWSSP) Mhe. Rais ameamua kuwaondolea adha wananchi zaidi ya elfu 30 wa kisiwani humo hivyo ni lazima mkandarasi huyo kwa kushirikiana na msimamizi watimize wajibu kwa kukamilisha mradi.
Awali, Mhandisi George Genes wa RUWASA alibainisha kuwa mradi huo umefikia asilimia 75 ya ujenzi na kwamba unahusisha ujenzi wa matanki 2, chanzo, ulazaji bomba, vituo 20 vya kuchotea maji na Uunganishaji maji kwa wananchi 200 walio ndani ya mita 30 na kwamba utanufaisha vijiji 7 vya kisiwani humo.
"Wewe ni mchapakazi kweli kweli yaani una muda mfupi Mwanza ila umeweza kufika kwenye kisiwa hiki wakati wengine hawakufika hapa kabisa, tunashukuru sana kwa mradi huu kwani wananchi wa Kome wameishi kwenye shida ya naji kwa miaka mingi." Mhe. Musa Abdalah, Diwani kata ya Bugoro.
Katika wakati mwingine Makalla ameridhishwa na uandikishaji wa wanafunzi wa awali na darasa la kwanza kwenye shule ya Msingi Muungano na ameagiza halmashauri kuweka mpango wa kuwa na chakula shuleni ili kutoa hamasa kwa watoto kuhudhuria masomo na kukamilisha ujenzi wa madarasa kutokana na uwepo wa maboma shuleni hapo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.