RC MAKALLA : OFISI YA MKUU WA MKOA KUPELEKA MADAKTARI BINGWA KUTOA HUDUMA YA AFYA HOSPITALI ZOTE ZA WILAYA
*RC Makalla aagiza Madaktari kuanza kutoa huduma za kibingwa kwenye Hospitali ya Buchosa*
*Awataka watumishi wa afya kufanya kazi kwa weledi kwa mujibu wa viapo vyao*
*Atoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali katika kutunza Miundombinu na vifaa tiba*
*Amshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya uboreshaji wa huduma za afya na maji*
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Daktari Thomas Rutachunzibwa kupanga utaratibu kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kupeleka madaktari bingwa katika hospitali za Halmashauri kwa kuanzia na Buchosa.
Mhe.CPA Amos Makalla ametoa agizo hilo mapema leo asubuhi alipofika kwenye hospitali ya Halmashauri ya Buchosa kukagua huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi zaidi ya Elfu 50 wa eneo hilo na kubaini ubora wa hali ya juu wa huduma hizo lakini mahitaji yakiwa kwenye huduma za kibingwa ambazo wamekua wakisafiri umbali mrefu kuzipata mjini Mwanza.
Mhe. Makalla amesema Rais Samia amekuwa kioo kwa kuwahudumia wananchi kwenye sekta ya afya na ndio maana kwenye halmashauri hiyo amepeleka fedha zaidi ya Bilioni 3 kujenga hospitali yenye hadhi ya mkoa hivyo ni lazima wasaidizi wake wampe ushirikiano kwa usimamizi mzuri wa ubora.
"Mwanzoni mwa ziara yangu ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kukagua miradi nikiwa wilayani Nyamagana nilitoa agizo kwa Mganga mkuu wa mkoa kushirikiana na Bugando kutoa huduma za kibingwa kwenye hospitali za halmashauri, sasa naagiza huduma hizo zije kuanza kutolewa hapa Buchosa." Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Makalla amewataka watumishi wa idara ya afya kutoa huduma bora kwa mujibu wa viapo vyao na wananchi kulinda Miundombinu ya hospitali hiyo na vifaa tiba ili viwasaidie kwa dahari ya miaka na kwamba atawasiliana na mamlaka husika kuhakikisha wanaongezewa watumishi kwenye hospitali hiyo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Sengerema Mhe Dominic Makoye amebainisha kuwa Chama hicho kinaridhika na huduma za afya zitolewazo kwa wananchi kwenye hospitali hiyo ambayo inahudumia zaidi ya wananchi 100 kwa siku katika hali ya ubora.
Naye, Mwenyekiti wa halmashauri ya Buchosa Mhe. Idama Kibanzi ametumia wasaa huo kutoa wito kwa wazazi kupeleka watoto shule ili wasome masomo ya sayansi na kuwa wataalamu wa afya kwenye siku za baadae ili kupunguza uhaba wa watumishi wa kada hiyo hapa nchini.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Buchosa Dkt. Daniel Matekele amefafanua kuwa halmashauri hiyo ina zaidi ya vituo 42 vya kutolea huduma za afya na kwamba jengo la huduma za dharula linasaidia kupunguza vifo kwa asilimia 40 kutokana na vifaa tiba vya kisasa na kwamba zaidi ya wagonjwa wanne walifikishwa hapo na kutibiwa.
Akikagua nradi wa maji kwenye kijiji cha Bupandwa unaosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhe. Makalla amewata wananchi kutunza chanzo na miundombinu ili huduma hiyo ipatikane kwa wananchi zaidi ya elfu 36 kwa sasa na elfu 80 baadaye.
Aidha, ameushukuru uongozi wa Sengerema na Buchosa kwa ushirikiano kwenye usimamizi wa fedha hizo zaidi ya Bilioni 7 na kufanikisha mradi kufikia hatua ya ukamilishaji ukitegemewa kuwa ifikapo mwezi Machi 2024 utakamilika kabisa na kutoa huduma kwenye vituo 120 vilivyotawanyika kwenye kata 3.
Akijibu hoja ya gharama za maji iliyoibuliwa na CCM wilaya hiyo CPA Makalla amewataka kutumia maji ya mradi huo ambayo ni safi na salama na kuacha kutumia maji ya ziwa ambayo yanawaweka kwenye adha ya kuliwa na mamba na kwamba gharama yake itakuwa ya chini sana kutokana na namna mradi ulivyotekelezwa kwa kisasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.