RC MAKALLA: VIWANJA NA. 194 NA 195 KITALU U, RWAGOSORE NI MALI YA SERIKALI
*Asimamisha ujenzi uliokuwa ukiendelea baada ya kampuni inayojenga kukaidi agizo la Mkurugenzi wa jiji*
*Asema umilikishaji wa viwanja uligubikwa na Ukiukwaji wa Sheria za nchi*
*Athibitisha uchunguzi umekamilika na wote waliohusika na uazaji na umilikishaji viwanja hivyo watafikishwa katika vyombo vya sheria*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CPA Amos Makalla amemtaka anayejenga kwenye viwanja namba 194 na 195 Kitalu U Mtaa wa Rwagosore Jijini Mwanza kusimamisha Ujenzi na kuondoka mara moja kwani Viwanja hivyo ni Mali halali ya Serikali na si vinginevyo.
CPA Makalla ametoa agizo hilo mapema leo Agosti 10, 2023 alipofika kwenye eneo hilo katika kufuatilia Utekelezaji wa Agizo la Serikali la Julai 20, 2023 lililomtaka anayejenga kusitisha kazi zote kufuatia umilikishaji wake kugubikwa na ukiukwaji wa sheria ya ardhi na taratibu za nchi.
"Tarehe 20 mwezi wa Saba mlipewa taarifa ya kusitisha ujenzi lakini mmekaidi na mmekua mkiendelea na ujenzi usiku na mchana sasa nimekuja kuwaambia kwa mara ya mwisho kwamba Muondoka na kuanzia leo jengo hili litakua chini ya Usimamizi wa jeshi la polisi." Mhe. Mkuu wa Mkoa.
Amesema Uuzwaji wa Viwanja hivyo uligubikwa na Mizengwe iliyopelekea mgogoro ambapo Serikali iliunda Kamati iliyopendekeza kufanyika kwa taratibu za Urejeshwaji wa Hati iliyomilikishwa baada ya kughushi nyaraka za Serikali na ujenzi ulisimame.
"Hili jambo la viwanja namba 194 na 195 kwenye Kitalu U Mtaa wa Rwegosore linajulikana na kamati iliundwa na ikatolea Mapendekezo ambayo serikali inaendelea kuyatekeleza katika kuhakikisha mgogoro huu unafika mwisho." Mhe. Makalla.
Aidha, Mhe. Makalla amebainisha kuwa wote waliohusika kughushi nyaraka kwenye umilikishwaji wanachukuliwa hatua kutokana na utovu wa nidhamu na kwamba tayari Kamati ya Mipango Miji ilishavunjwa na unafanywa mchakato wa kuunda kamati ingine.
"La kwanza Viwanja hivi 194 na 195 (Kitalu 7 Rwegosore) ni mali halali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mchakato wa umilikishaji kwa anayejenga ulikiukwa na ulikua batili na ndio maana tunaendelea na mchakato wa kurejesha Hati" Amesisitiza Mhe. Makalla.
Vilevile, amefafanua kuwa TAKUKURU waliagizwa kuchunguza sakata hilo ili wote waliohusika kwenye suala hilo ovu wachukuliwe hatua na taratibu zinaendelea ambapo wakati wowote waliohusika watafikishwa Mahakamani.
"Umilikishwaji wa Mmiliki huyu haukua halali ulikumbwa na Miizengwe na mimi kama Mkuu wa Mkoa nipo kusimamia amani kwenye eneo langu na nitahakikisha ninalinda Mali za Serikali.
"Kuanzia sasa eneo hili litalindwa saa 24 na jeshi la Polisi na tusione mtu yeyote anaendelea na kazi baada ya tamko langu hivyo nataraji hakutakua na mtu yeyote anafanya kazi kwenye eneo hili." Amesisitiza Makalla
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.