Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka washiriki wa mafunzo ya Dawati la Jinsia na Ushauri Nasihi kuhakikisha wanaielewa mada ya Unyanyasaji wa kijinsia na kuhakikisha wanakwenda kuitokomeza katika jamii zao.
Mhe. Malima ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya Dawati la Jinsia na Ushauri Nasihi yaliyofanyika katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Tawi la Mwanza leo Machi 27,2023.
"Kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia uanze na mimi,na wewe ili jamii ipate uelewa na ishiriki juhudi za kuondokana na hali hiyo," amesema Mhe.Malima.
Aidha, ametoa wito kwa menejimenti za Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya juu Nchini, ambavyo bado hawajaanzisha madawati ya haya na kutoa mafunzo ya Ushauri na jinsi ya kusimamia madawati haya, kufanya hivyo haraka kwani itasaidia sana kutokomeza vitengo vya unyanyasaji wa jinsia na hivyo kuisaidia jamii kwa ujumla.
Hata hivyo,ameongeza kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo ndani ya Chuo hicho kumekuja wakati muafaka ambako jamii sasa inaanza kuwa na uelewa mpana wa masuala ya Jinsia na Ushauri Nasihi.
"Kuandaa jambo hili siyo kazi rahisi, hivyo ninaupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania Chini ya Makamu Mkuu wake Profesa Elifas Bisanda, akisaidiwa na Kurugenzi ya Huduma za Wanafunzi na Mkurugenzi wa kituo cha Mwanza kwa maandalizi yote na kuona umuhimu wa kutoa mafunzo haya ya Ushauri Nasihi kwa jamii yake,"amesema Mhe.Malima.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa Elifas Bisanda amesema Chuo hicho kitaendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza kwa kuwapa elimu wafungwa wenye nia ya kujiendeleza ili nao waweze kutimiza ndoto zao.
Naye, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania huduma za mikoa, Profesa Alex Makulilo amesema wamekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wa kumudu changamoto mbalimbali, sababu wafanyakazi wengine wanakwenda kufanya kazi katika Taasisi nyingine pia wengine huwa ni waajiriwa wapya ambao hawajajengewa uwezo hivyo wamekuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo mara kwa mara.
Serikali ilitoa mwongozo wa uanzishwaji wa Dawati la Jinsia katika Taasisi za Elimu ya juu na Elimu ya Kati, hivyo amewapongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali katika kuanzisha madawati hayo.
Akimshuku Mhe.Malima kwa niaba ya washiriki wote Dkt.Regina Malima amesema wamefarijika sana kwa kuwa na mtendaji Mkuu wa Mkoa na hivyo wanaahidi yale yote yatakayofundishwa watakwenda kuyafanyia kazi kwa manufaa ya Umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.