Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ameziagiza taasisi zinazosimamia Sekta ya Maji mkoani humo kuweka mikakati madhubuti ya kumaliza kero ya uhaba wa Maji kwa wananchi kwa kuongeza uzalishaji na usambazaji wa huduma hiyo muhimu.
Mhe. Malima amesema hayo leo Septemba 16, 2023 wakati wa Kikao chake na Taasisi za Sekta maji Mkoani humo kilichokutana kuweka mipango, mifumo na mikakati ya upatikanaji wa Maji ya kutosha ili kumaliza adha ya uhaba wa maji kwa wakazi hasa waishio kwenye naeneo yenye miinuko mkoani humo.
"Nilipozunguka kwenye maeneo mbalimbali katika ziara zangu za kujitambulisha na kusikiliza kero za wananchi jambo la maji limekua ni kilio cha wengi, nataka tumalize tatizo la maji tena sio kwenye makaratasi bali wananchi wahisi kabisa kuwa tatizo la Maji limekwisha."
Vilevile, amewaagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) kufanya tathmini ya kina ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi na wachukue hatua ya kuongeza uzalishaji na usambazaji wa maji ili wananchi wengi wapate maji ya kutosha kukidhi mahitaji ya kila siku.
Aidha, Malima amewataka wataalamu hao kufanya uchunguzi wa hali ya vifaa kutoka kwenye chanzo kikuu cha maji cha Kapripoint ili kubaini changamoto na kuweza kuzitatua kwa kuokoa upotevu wa maji na kuongeza uzalishaji na usambazaji wa huduma hiyo kwa wakazi ndani ya siku 14.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Robert Luboja amefafanua kuwa taasisi hiyo inaendelea na jitihada za kuongeza uzalishaji na usambazaji wa Maji kwa kuongeza mitambo na vifaa kama kota kwenye chanzo kikuu na kwamba hadi kufikia mwezi Oktoba kutakua na mabadiliko makubwa na wananchi wataona tofauti na kwamba kwa sasa taasisi hiyo inakusanya wastani wa Shilingi Bilioni 2.1 hadi 2.4 kwa mwezi.
Vilevile, amesema kwa siku za karibuni taasisi hiyo imejipanga kuwekeza kwenye vifaa vya kisasa na kukarabati Miundombinukuwa ya maji na kwamba wamekusudia hadi kufikia Juni 2023 upotevu wa Maji utapungua kutoka asilimia 32 hadi 20 na kwamba wataongeza wateja kutoka elfu 94 kwenye maeneo ya mjini waliopo hivi sasa.
Awali, Meneja Msaidizi Kitengo cha Mitambo na Uzalishaji MWAUWASA, Mhandisi Joseph Shillinde alifafanua kuwa Mitambo ya chanzo kikuu cha Maji ina uwezo wa kuzalisha lita Milioni 108 kwa siku lakini kutokana na uchakavu ni lita Milioni 90 kwa siku pekee zinazalishwa kuwahudumia wananchi wenye mahitaji ya lita milioni 160 kwa siku.
Mhandisi, Emmanuel Mafuru, Kaimu Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mwanza amefafanua kuwa kwenye maeneo ya Vijijini ndani ya wilaya tano za Mkoa huo kuna Miradi inayoendelea kutekelezwa ya Shilingi Bilioni 112 inayotarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2023 na kwamba itakapokamilika itawanufaisha zaidi ya laki nne na itaongeza mtandao wa wanufaika kutoka 67%
Naye Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Maji Mji wa Sengerema (SEUWASA), Mhandisi Sadala Hamis amesema katika Mji wa Sengerema kuna chanzo kimoja kinachozalisha lita Milioni 5 kwa siku na kwamba wakazi wapatao takribani 166,500 wanahudumiwa ambapo kwa wakazi wote wa Mji huo na makusanyo yao ni Milioni 110 kwa mwezi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.