Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amelipongeza Shirikisho la Wachimba Madini nchini FEMATA kwa kupiga hatua na kutoa mchango kwenye Pato la Taifa na kuwakumbusha kutanguliza maslahi ya nchi kwa kuzingatia utunzaji wa Mazingira.
Akizungumza na uongozi na wanachama wa Shirikisho hilo kwenye ufunguzi wa wiki ya Madini inayofanyika kwenye viwanja vya Rock City Mall Jijini Mwanza,Mkuu huyo wa Mkoa amesema anashuhudia mabadiliko ya wachimbaji wadogo hapa nchini kuanzia kwenye vifaa,ajira,kuelimika na mshikamano uliopo miongoni mwao ambao umekuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.
"Bwana Rais wa FEMATA John Bina niseme ukweli kutoka moyoni kwangu hongereni sana kwa hatua mnayopiga,hata mimi nilivyokuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini nikiwa Bungeni nilianzisha kauli ya kuwaita wachimbaji wadogo na siyo wachimbaji wadogo wadogo maana yangu ni watu mnaokwenda hatua kwa hatua hadi kuwa wachimbaji wakubwa"amesema Mhe.Malima
Amewakumbusha FEMATA kuwa wakereketwa wa utunzaji wa Mazingira nchini hasa kutokana na uhalisia wa shughuli zao,kwani wapo baadhi yao hawazingatii hilo na badala yake wanaharibu Mazingira kuanzia kutiririsha maji yenye kemikali ambayo yana hatarisha afya za watanzania,amewahimiza Shirikisho hilo kulipa kipaumbele jambo hilo ili liwe na matokeo chanya.
"Mhe.mgeni rasmi maagizo yako yote tumeyapokea na kukuahidi kuyafanyia kazi,hii wiki ya Madini miongoni mwa mambo tunayofanya ni pamoja na kutoa elimu kwa wanachama wetu ikiwemo utunzaji wa mazingira"John Bina,Rais wa FEMATA.
"Serikali kwa kuendelea kutambua mchango wa Wachimba Madini imeweka mazingira mazuri kwao ya ufanyaji wa shughuli zao ikiwemo kuondoa changamoto zilizokuwa zinarudisha nyuma au kuchelewesha shughuli zao,ndiyo maana sasa wanazidi kupiga hatua na kuwa nguzo ya pato la Taifa" Francis Mihayo,Kamishna wa Madini.
Shirikisho la Wachimba Madini nchini kwa mara ya kwanza linafanya Mkutano wao Mkuu na wiki ya Madini Mkoani Mwanza inayokwenda pamoja na kongamano lenye lengo la kuelimishana na kuzijadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kushauriana namna ya kuzitatua na pia kutoa
ushauri na maoni yao Serikalini kuhusu kuyaboresha mazingira yao ya kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.