Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima ameivunja Kamati ya usimamizi ya ujenzi wa Jengo la abiria la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwanza kutokana na ubadhirifu wa fedha za Mradi huo.
Akizungumza leo na wahusika wa Mradi huo wa Jengo la abiria mara baada ya kulifanyia ukaguzi Mkuu huyo wa Mkoa amesema baada ya kuivunja kitakachofuata ni kupata taarifa za kina za kila muhusika ili kujirudhisha uwezo wao.
"Hainiingii akilini kuona taarifa inayosema Mkandarasi Mshauri Berno Balinamomi amepata kazi hiyo bila mkataba kwa zaidi ya Shilingi milioni mia moja na kufanyika malipo yaliyopitiliza gharama halisi" amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Amesema huyo Mkandarasi Mshauri licha ya kulipwa pesa nyingi amefanya makosa mengi katika ujenzi huo kiasi cha kupoteza sifa ya Jengo hilo kuwa na hadhi ya Kimataifa.
Amesema baada ya kuivunja Kamati hiyo atashirikiana na Katibu Tawala wa Mkoa Balanda Elikana kuunda Kamati mpya itakayowashirikisha Wataalamu wa ujenzi na viongozi wa vyombo vya Ulinzi na usalama.
Mhe Malima amemtaka Mkandarasi huyo kurekebisha kasoro zote na Jengo hilo kumalizika haraka ili Mkoa wa Mwanza ambao upo Kimkakati upokee Watalii wanaozidi kuvutiwa na Vivutio vingi vya Kitalii vilivyopo Mkoani humo na Mbuga ya Serengeti.
Jengo la abiria lenye gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 13 linalojengwa kwa kuchangiwa gharama na Halmashauri mbili za Nyamagana iliyotoa zaidi ya Shilingi Bilioni 2 na Ilemela iliyotoa zaidi ya Shilingi Bilioni 1 na nyingine kuongezwa na Serikali Kuu hadi sasa zimeshatumika Shilingi Bilioni 8.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.