Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amewapongeza wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari kwa uwakilishi mzuri kwenye Mashindano ya Michezo ya Shule za Msingi na Sekondari ambapo Mkoa huo umeibuka Mshindi wa kwanza Kitaifa kwa Michezo ya UMITASHUMTA na wa Pili kwa UMISETA.
Mhe. Malima amesema hayo leo Agosti 29, 2022 wakati wa hafla ya kukabidhi vikombe 16 vya ushindi kwa michezo mbalimbali ya wanafunzi kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISETA) kufuatia michezo iliyofanyika Kitaifa Mkoani Tabora mapema mwezi Agosti 2022.
"Napenda niwapongeze sana kamati nzima kuanzia walimu waliofanya maandalizi, wadau wetu, mameneja na waratibu wote lakini pongezi zangu za dhati kabisa ni kwa wanamichezo wenyewe waliotuletea vikombe hivi leo." Malima.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi kuendeleza vipaji vya watoto wao na kuwaendeleza kila wanapoonesha uwezo kwenye michezo kadhaa ili kukuza vipaji na kuwafanya wanafunzi kuwa wachezaji wazuri wanapomaliza shule na kuweza kujiimarisha hata kiuchumi kupitia michezo mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amewapongeza walimu na wanafunzi wote walioshiriki maandalizi na Mashindano ya shule za Msingi na Sekondari mkoani humo na ametoa rai kwao kuendelea mbele katika nyanja za kitaaluma kupitia chachu ya Michezo hiyo.
"Ninafurahi kuwa juhudi zenu zimetufikisha hapa na ni matumaini yangu kuwa ushindi kwenye michezo tutautafsiri kwenye matokeo mazuri kitaaluma katika kila shule mkoani hapa" Amesema, Mwalimu Elias Nkwabi, Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza.
Afisa Michezo Mkoa wa Mwanza, William James amesema wanafunzi 240 wameshiriki michezo hiyo Kitaifa Mkoani Tabora na kushika nafasi ya Kwanza kwa michezo ya UMITASHUMTA na nafasi ya pili kwa UMISETA ikiwa ni matunda ya maandalizi mazuri yaliyofanywa na kamati na Mashindano.
Kupitia hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa amekabidhiwa vikombe vya ushindi kupitia michezo ya Ngoma, Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Kikapu wavulana, Kwaya, Riadha Wavu wavulana, wavu wasichana, Soka wasichan, Riadha wasichana, Mpira wa Mikono wavulana na Kikombe cha ushindi wa jumla kwa UMITASHUMTA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.