Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amekipongeza Chama cha Madaktari wa Tiba za Wanyama nchini TVA kwa kuyatumia Maadhimisho ya Kitaifa Mwanza ya siku ya utoaji huduma za afya ya wanyama, kwa kutoa elimu shuleni kuwahamasisha wanafunzi wa kike kuchangamkia taaluma hiyo.
Akizungumza kwa niaba yake leo wakati wa ufungaji wa Maadhimisho hayo kwenye viwanja vya Furahisha,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Masala amesema kumekuwa na kasumba ya mfumo dume kuwa kazi hiyo ni ya wanaume kutokana na kuwakabili wanyama wengine wenye ukali na nguvu,jambo ambalo halina ukweli wowote.
"Tumemshuhudia Rais wetu Mhe.Dkt.Samia Suluhu akiweka mazingira mazuri ya kuwepo na shule maalum za wasichana kuchukua masomo ya Sayansi,hii maana yake ni kutaka kuwepo na uwiano mzuri wa wataalamu wa kike wa kulijenga Taifa letu".Amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Amewakumbusha pia wakazi wa Mwanza wenye mifugo kuyachangamkia Maadhimisho hayo kwa kupata elimu ya kutosha na kuona umuhimu wa chanjo za mara kwa mara za mifugo yao ili iwe salama kwa mlaji na uhakika wa soko.
"Ndugu mgeni rasmi mbali ya kuhamasisha elimu hiyo shuleni,April 27 tumetoa huduma mbalimbali za mifugo bila malipo zikiwemo chanjo na upasuaji na kufikisha idadi ya mifugo 607 tuliyohudumia siku hiyo maeneo ya Kisesa wilayani Magu,lengo likiwa ni kuwaelimisha wananchi kuwa na mifugo bora wakati wote,"James Kawamala,Katibu wa TVA Taifa.
"Maadhimisho haya Kitaifa tumeyafanya kwa mara ya kwanza na tukachagua Mkoa Mwanza ambao una sifa ya kuwa na wafugaji wengi,hivyo tumefarijika elimu tuliyotoa itakuwa na tija kwao na Taifa kwa ujumla," Prof.Esron Karimuribo,mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Kila ifikapo wiki ya mwisho ya April,Tanzania hujumuika na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku ya utoaji huduma za afya ya wanyama ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni Kukuza utofauti,usawa na ushirikishwaji katika taaluma ya tiba ya wanyama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.