Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amemtaka Mkandarasi anayejenga Mradi wa Soko Kuu la Kisasa Mohamed Builders Company Limited na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuweka mipango thabiti ya kukamilisha Mradi huo ili kuepusha gharama zisizotarajiwa endapo utatakelezwa kwa muda mrefu zaidi na uweze kuwahudumia wananchi kwa haraka.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo sokoni hapo Septemba Mosi 2022 alipoungana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza Mhe. Anthony Dialo kwenye ziara ya kukagua Ujenzi wa Miradi ya Kimkakati.
"Mimi binafsi nimeridhishwa sana na mpango wa mradi huu maana una nia ya kupandisha maisha ya wananchi kuwa ya kisasa na tumeona kuwa umegharimu zaidi ya Tshs Bilioni 20, hizi fedha nyingi sana hivyo basi huduma zitakazotolewa hapa ni lazima zilenge kuwasaidia wananchi hasa wafanyabiashara wadogo." Amesema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Mkuu wa Idara ya Kilimo na Ushirika Erick Mvati akimuwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji amefafanua kuwa zaidi ya Tshs Bilioni 20 zitatumika kujenga mradi huo ulioanza kutekelezazwa 0ktoba 2020 na utakamilika ifikapo Septemba 30 2022 na kwa sasa umefikia asilimia 79 ya utekelezaji.
Aidha, amefafanua kuwa Mradi huo ulioajiri zaidi ya vijana 100 wakati wa utekelezaji, utasaidia kuongeza mapato kwenye Halmashauri hiyo na kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu kutokana na huduma kadhaa zitakazokuwemo zikiwemo mabenki, vizimba vya wafanyabiashara wadogo, eneo la wafanyabiashara wakubwa, michezo ya watoto na eneo la kuegesha magari zaidi ya 150.
Baada ya ukaguzi huo viongozi hao wamefika kwenye Bandari ya Mwanza Kusini na kukagua Ujenzi wa Meli kubwa ya kisasa ya MV Mwanza yenye uwezo wa kubeba Magari madogo 20, makubwa 3, tani 400 za mizigo na Abiria 1200 kwa wakati mmoja ambayo inatekelezwa na Mkandarasi Gas Entec kutoka Korea Kusini kwa Bilioni 70 wamepongeza utekelezaji wa Mradi huo na wamesisitiza ukamilishaji wa ujenzi huo kwa manufaa ya wananchi waishio kwenye ukanda wa maziwa makuu.
"Ujenzi wa hii Meli ulianza January 2019 na ulikua uende kwa miaka miwili lakini zilitokea changamoto nyingi ambapo mkataba uliongezwa hadi Mei 2023 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 71 ya ujenzi na hakuna meli kubwa kama hii kwenye ukanda wa maziwa makuu." Amefafanua Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli, Erick Hamisi
Bwana Hamisi ameongeza kuwa Meli hiyo inajengwa kwa Tshs Bilioni 97 ambapo Chelezo yake imegharimu Bilioni 36 na mradi huu umeajiri watanzania 150 hadi 200 na wataalamu 6 tu kutoka nje na ifikapo Oktoba mwaka huu meli hii itaingizwa kwenye maji ambapo matengenezo mengine yataendelea ikiwa kwenye maji.
"Nimefarijika sana leo, awali wakati Mradi huu unaanza tulipokua na Michoro tu kwenye makaratasi ulikua ukisikia zile takwimu unadhani ni utani Rais Samia anatengeneza Miundombinu kwa ajili ya wananchi wake na hiyo ndio dira yake ya kuwatumikia wananchi na kwakweli ameamua kuhakikisha mambo hayasimami hivyo basi wananchi wa Mwanza wakae Mkao wa kusafiri nayo." Malima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.