Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima ametoa wito kwa Wadau wa Usalama barabarani kuangalia namna ya kufanya mabadiliko kwenye baadhi ya Sheria za Usalama barabarani ili ziweze kutoa adhabu kali zaidi kwa wote watakaosababisha ajali kwa uzembe.
Mhe. Malima amebainisha hayo mapema leo Machi 17, 2023 wakati wa hafla ya Kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama barabarani Kitaifa yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza kuanzia tarehe 14 Machi, 2023 ambapo yalifunguliwa na Mhe. Waziri Mkuu wa Tanzania.
"Ajali nyingi za Barabarani zinatokea kutokana na uzembe wa kujitakia kama kuendesha vyombo vya moto kwa muda mrefu bila kupumzika, kuendesha chombo wakati umelewa na mwisho kusababisha vifo vya raia na kupoteza nguvu kazi ya Taifa" Mhe. Malima.
Vilevile, ametoa rai kwa waendesha Pikipiki za abiria (Bodaboda) kuzingatia sheria za Usalama wawapo kwenye shughuli zao kwani eneo hilo limekua chanzo kikubwa zaidi cha ajali na kwa askari wa barabarani amewataka kuwajibika ipasavyo ili kulinda maisha ya wananchi.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi amebainisha kuwa pamoja na Jeshi la polisi kutembelea Shule za Msingi na Sekondari, makundi mbalimbali ya watumia vyombo vya moto Mkoani humo wamepewa Elimu ya Usalama barabarani.
Naye, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mabaraza ya Usalama barabarani ambaye pia ni mwenyekiti wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni Idd Azzan ametumia wasaa huo kulihakikishia Jeshi la Polisi na wananchi kuendelea kutoa elimu ya Usalama barabarani kila wakati ili kuhakikisha jamii inakumbushwa wakati wote juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria za Usalama kila watumiapo barabara.
"Nia yetu kubwa ni kuhakikisha ajali kama hazitaondoka kabisa basi zinapungua hivyo nawasihi watumiaji wa Miundombinu ya barabara kufuata sheria za usalama ili kuhakikisha wanakua salama barabarani na waweze kuwalinda watumiaji wengine wa barabara." Amesema mwenyekiti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.