Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka Wadau wa Utalii kuhakikisha wanatangaza vivutio vya Utalii vinavyopatikana katika Mkoa huo ili kuwaleta watalii wengi zaidi katika vivutio mbalimbali siyo Serengeti na Ngorongoro peke yake.
Mhe.Malima ameyasema hayo leo Septemba 6, 2022 alipokutana na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wadau wa Utalii alipowaita ili kuwapa mbinu, mikakati na namna bora ya kuboresha na kuinua Sekta hiyo.
"Lengo langu ni kutaka kuangalia kila mtu anauza nini, na kwa umoja wetu tuuze nini, ili mwisho wa siku tuunganishe nguvu ya pamoja katika kuutangaza utalii wa Mwanza,"alisema Mhe.Malima.
Mhe.Malima ameeleza kuwa Mwanza ni lango la kuingia Hifadhi ya Serengeti ambapo haichukui zaidi ya saa mbili kwa gari,pia alieleza ukaribu wa Mwanza na mbuga za Rumanyika, Kyerwa,Burigi- Chato,Kigosi na Rubondo.
Aidha, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane ACC. Eva Mallya amesema kunatakiwa kuwa na namna nzuri ya kutangaza Mwanza kwa kuwa na kipeperushi au Jarida ambalo litaonesha vivutio vyote vilivyopo Mwanza kwa pamoja.
"Tuunganishe vivutio (packagies) hii itasaidia watalii wanaokuwepo Mwanza kuweza kutumia muda zaidi kuliko kuuza kivutio kimoja kimoja, kunakosesha thamani ya eneo,ni rahisi kukuza Saanane kwa kujumlisha na vivutio vingine mfano Bujora,"alisema Mallya.
Naye, Mkuu wa Idara ya Utalii Kanda ya Ziwa Dainess Kunzugala amesema Suala la utalii linategemea utayari wa miundombinu (airport) huduma za malazi pia linategemeana ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi, hivyo kuna umuhimu wa kuunda umoja wa wadau wa utalii (Association) kwa kanda ya ziwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Rubondo ACC.Moranda B.Moranda ameeleza kuwa wadau wote wa Utalii wanatakiwa kuangalia namna wanavyoweza kuwahifadhi wageni kwa upande wa vyakula, malazi na Gharama za Utalii na huduma mbalimbali kwani kwa kufanikisha hayo wanaweza kupokea watalii wengi zaidi kutoka sehemu mbalimbali.
"Tusimtazame mtalii kama tunavyojitazama sisi..... nahitaji kuoga naletewa maji kwenye ndoo...hii hatutafanikiwa, tutoke huko," alisisitiza Mhe.Malima.
"Katika hali ya kufanya Utalii wa Mwanza tufanye kama wanavyofanya wenzetu,tusifanye kama tulivyozoea wenyewe," ameongeza Mhe.Malima
Kwa upande wake, Kamanda Kikosi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe ACC Yustin Njamas amesema kuwa Viongozi wakielewa kuhusu swala hili la utalii watafanikiwa sana kwa sababu watapata ushirikiano mkubwa kutoka kwao na watakuwa na mafanikio makubwa.
Aidha,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ibanda ACC. Fredrick Mofulu amesema tangu mtalii anapokelewa kuwe na uangalizi wa moja kwa moja lazima kuwe na utaratibu wa uangalizi na uwezo mkubwa wa kupokea wageni na kuwahudumia kwa ubora wa viwango pendekezwa kwa watalii.
Mmoja kati ya Wafanyabishara wakubwa Mwanza Bwana Joel Charles Makanyaga amesema kuwa Jiji kubwa la Mwanza linapitika kwa njia zote wadau wa Sekta ya Utalii wanatakiwa wakae kwa pamoja ili waje na mpango wa pamoja ili kukuza uchumi na utalii wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.