Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amesema Jiji hilo linazidi kukua kiuchumi kutokana na rasilimali zilizopo na kuwa kitovu cha Biashara eneo la Nchi za Maziwa Makuu.
Akizungumza leo kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Maafisa wanafunzi wa Majeshi ya ulinzi wanaosoma Chuo cha ukamanda na unadhimu Duluti Arusha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Uchumi wa bluu unaotokana na Ziwa Victoria umechangia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Viwanda kwa ujumla.
Amesema kuondokana na uvuvi wa kawaida unaotumia nguvu nyingi na kupata samaki wachache, sasa wamepiga hatua kwa Wananchi kuelimishwa kutumia uvuvi wa kisasa na Ufugaji Samaki kwenye Vizimba kwa kufuga kwa muda mfupi na kupata faida kubwa.
"Kwa kutambua Mwanza ni Mkoa wa kimkakati Serikali ya awamu ya Sita imeleta Miradi mingi mikubwa ukiwemo ujenzi wa soko la kisasa la Kimataifa, Ujenzi wa Reli ya kisasa
(SGR) ambayo itarahisisha shughuli za kiuchumi na kufanya uzidi kukua", amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Mhe Malima amesema kutokana na soko zuri la Samaki huko barani Ulaya na shughuli za Utalii, ukarabati wa uwanja wa kisasa na wa kimataifa wa ndege unaendelea ili kuruhusu ndege kubwa za kimataifa za mizigo na abiria kufanya shughuli zake za kibiashara Mkoani humo.
Awali akizungumzia lengo la ziara yao ya mafunzo Mkoani Mwanza, Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC) Duruti Brigedia Generali Sylvester Damiani amebainisha wametambua Mkoa huo una mambo mengi ya kujifunza ya kiuchumi na Kijamii pia kupakana na nchi jirani watajifunza mikakati ya kujiimarisha kiulinzi na changamoto zake hivyo siku nne watakazokuwa hapo wataelimika vizuri na kushauri pia.
Aidha, amesema Chuo hicho kinatoa mafunzo ya kijeshi na uongozi ngazi ya Diploma, Degree na Sayansi ya kijeshi kwa Maafisa hao ili kuwaandaa kwenda kushika nyadhifa za juu kwenye majeshi yao.
"Ziara yetu imebeba Kauli mbiu ya Amani na Usalama kwa Maendeleo Endelevu tutapata somo zuri tutakapo kuwa kwenye ziara hii kwenye Wilaya za Ilemela, Nyamagana na Misungwi," amesisitiza Bregedia Generali Damiani.
Mkuu wa Mkoa akijibu swali kutoka kwa Meja Abduwelly Isack kutoka Kenya kuhusiana na mkakati wa Mwanza kuinua zao la Pamba amesema Serikali ya awamu ya Sita imeaimarisha Vyama vyote vya Ushirika ambavyo awali havikusimamia ipasavyo,pili imemuinua mkulima kwa kuboresha bei nzuri ya Pamba, kumpatia mbegu bora pamoja na mbinu za ulimaji wa kisasa.
Meja Lydia Damas kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ametaka kujua Maendeleo ya Uchumi wa bluu na suala la usalama kwa wavuvi Ziwani, Mhe Malima amesema usalama upo wa kutosha hasa kutokana na kuimarisha doria na kuwashughulikia wachache waliojitokeza kufanya uharamia pia Wananchi wameshirikishwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama wanapotokea watu wenye kutiliwa shaka.
Malima ameongeza kuwa Viwanda na Wananchi wanaendelea kuelimishwa kupitia Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kuhusu utunzaji wa Ziwa Victoria kuepuka kutiririsha taka ambazo zinakwenda kuua mazalia ya samaki na kuleta madhara kwa afya ya mwananchi kwa ujumla.
Maafisa hao wanafunzi wanatoka nchi marafiki na Tanzania ikiwemo Kenya, Uganda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Nigeria, India na Misri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.