Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewahimiza Wananchi wa Mwanza kujenga mshikanano ili timu ya soka ya Pamba FC inayoshiriki ligi ya Championship ishinde mchezo wake wa nyumbani dhidi ya Kitayose siku ya Jumamosi na ipande ligi kuu msimu ujao.
Akizungumza na Vyombo vya habari za michezo ofisini kwake leo kwa lengo la kuwahamasisha wana Mwanza kuelekea mchezo huo dhidi ya Kitayosa,amesema mchezo wa soka hauna miujiza zaidi ya mikakati mojawapo ni wananchi kufurika kwa wingi uwanja wa Nyamagana wanawake kwa wanaume hali ambayo itawaongezea ari wachezaji na hatimaye kutoka na ushindi.
"Niombe nitumie nafasi hii kwa wana Mwanza tujitokeze kwa udi na uvumba katika mchezo huo na hii iwe kwa michezo yote ya nyumbani ukiwemo ule wa Mashujaa FC utakaochezwa Aprili 15 mwaka huu hapo uwanja wa Nyamagana".Amehimiza Mhe.Malima
Amewakumbusha wananchi wa Mwanza wasiwe wazito kuichangia kwa hali na mali timu hiyo kwani kuendesha timu ni gharama na matokeo ya kuipandisha na kucheza ligi kuu yatakuwa na faida kwa wananchi wote wa Mkoa huu ikiwemo burudani ya kuzishuhudia timu mbalimbali na pia kiuchumi.
Tayari Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ni mkereketwa wa michezo nchini mwenye sifa ya kuipandisha timu ligi kuu kwenye Mikoa aliyofanya kazi,amesha nunua tiketi 500 na kufanya jumla ya tiketi zilizonunuliwa na wadau wa michezo kufika 1500 ukiwa ni mkakati wa kuwahamasisha wana Mwanza kufurika kwenye dimba la Nyamagana
"Niwakumbushe pia uongozi wa Pamba endapo tutafanikiwa kucheza ligi kuu msimu ujao ni lazima waweke mipango madhubuti kwa kila msimu kuwepo na malengo fulani ili kuhakikisha tunaendelea kubaki tofauti na hapo tutaishia kupanda na kushuka".RC Malima
Katika msimamo wa ligi ya Championship timu ya soka ya Pamba ipo nafasi ya tatu na pointi zake 47 kibindoni huku Kitayose FC kutoka Tabora ikishikilia nafasi ya pili na mtaji wa pointi 49 huku kinara wa ligi hiyo ambao wamejiweka nafasi nzuri ya kupanda ligi kuu msimu ujao ni wafunga buti wa JKT Tanzania wakitamba na pointi 56 kileleni.
Pamba FC iliyotamba miaka ya nyuma kuwatoa wachezaji waliokuja kuwa nyota wa timu za Simba na Yanga wakiweno George Masatu,Hussein Marsha , Fumo Felician na marehemu Beya Simba ina miaka 22 haijacheza ligi kuu ya Tanzania Bara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.