Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewakaribisha wananchi wote wa mikoa ya jirani kuja kumpokea kwa shangwe Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Mpango atakapowasili Kijiji cha Hungumalwa Wilayani Misungwi kesho asubuhi akitokea Mkoani Shinyanga.
Akizungumza leo katika mkutano na Vyombo vya Habari kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Mhe.Malima amesema mara baada ya kumpokea Makamu wa Rais ataelekea kwenye mradi wa Uzalishaji wa ng'ombe bora wa maziwa na nyama kwenye shamba la Mifugo la Mabuki lililopo Wilayani Misungwi.
"Hapo kwenye mradi wa Uzalishaji wa ng'ombe bora wa maziwa na nyama napenda kuwaona wananchi wengi kwani kuna mengi na muhimu ya kujifunza namna ya ufugaji wa kisasa na siyo uchungaji,kuchunga ni kutembea na ng'ombe umbali mrefu bila ya kuwa na tija yoyote".Amesisitiza Mhe.Malima.
Amesema lengo la Mkoa wa Mwanza ni kuwahamasisha wananchi kuwa wafugaji bora na mifugo yao iwe na tija kwa maziwa na nyama,pia itakuwa faida kwenye viwanda vya nyama kwa kupata ngo'mbe bora.
"Namshukuru Mhe.Rais kwa kutuletea ng'ombe bora 500 ambao wataleta matokeo chanya ya kupata ng'ombe bora,vilevile wapo Vijana 85 wanaoendelea kupata utaalamu wa ufugaji bora hapo Mabuki."Mhe.Malima.
"Sisi kama Wizara kwanza tunamshukuru sana Mkuu wa Mkoa Mhe.Malima kwa kutambua umuhimu wa shamba hilo la mifugo na kuliingiza kwenye ratiba ya Makamu wa Rais,mpango wetu ni kulifanya shamba hilo kuwa la mfano ukanda huu wa Afrika Mashariki."Mhe.Abdallah Ulega Waziri wa Uvuvi na Mifugo.
Aidha, Makama wa Rais Mhe.Dkt.Philip Mpango siku ya Jumatano saa mbili asubuhi atafungua kikao cha tathmini ya utendaji wa shughuli za Mahakama ya Tanzania kwenye ukumbi wa mikutano Malaika Beach Resort,baada ya hapo atapata wasaa wa kuwasalimia wananchi eneo la Buswelu Centre Wilayani Ilemela.
Akiwa njiani kurudi Dodoma Mhe.Mpango atasimama eneo la Kisesa Wilayani Magu na kuwasalimia wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.