Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka wachezaji wa timu ya soka ya Pamba inayoshiriki ligi ya Championship kucheza kwa malengo na hatimaye kupanda ligi kuu msimu ujao.
Akizungumza leo na wachezaji na uongozi wa klabu hiyo kwenye uwanja mkongwe wa Nyamagana Mkuu huyo wa Mkoa amesema mchezaji anayecheza bila ya malengo huyo hafai na aondolewe kwenye timu kwenye dirisha dogo.
"Kwangu mimi nina mambo mawili ambayo sikubaliani nayo kucheza bila malengo na migogoro mkinionesha hali hiyo najiweka kando nanyi", amesisitiza Mhe.Malima
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ameinua soka kwenye Mikoa aliyofanya kazi ya Mara na Tanga amesema hivi sasa anaendelea kutunisha mfuko wa kuendeleza soka Mkoani Mwanza na wadau wamekuwa na imani na mwendo wa timu ya Pamba hivyo amewataka wasimuangushe kwa kufanya mambo yasiyo na tija.
Aidha, Mhe. Malima kwenye Mkutano huo na wachezaji wa Pamba amewakabidhi Shilingi Milioni moja kama motisha baada ya kufanya vizuri michezo yao miwili ya ligi Daraja la kwanza kwa kuilaza Pan African bao 1-0 kabla ya kuibugiza Trans Camp mabao 2-0.
"Jiwekeeni utaratibu wa kucheza soka la kisasa na kutanguliza nidhamu hii ndiyo siri ya nyota wengii wa soka Duniani walivyofanya pia wekeni luninga kubwa kwenye hostel yenu mtakayotumia kuona mchezo mlioshiriki na kubaini makosa au sehemu mliofanya vizuri kuongeza zaidi maarifa, kwa kufanya hivyo mtawavutia wafadhili kutokana na kuwa na timu inayofanya vizuri wakati wote," Amesema Mkuu wa Mkoa.
Awali akimkaribisha Mhe. Malima, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano
wa klabu hiyo Aleem Alibhai amemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa moyo wa kupigania timu hiyo na kusisitiza motisha wanayopata kutoka kwa wadau inawaongezea ari ya kufikia malengo yao ya kucheza ligi kuu.
Timu ya soka ya Pamba katika msimamo wa ligi Daraja la kwanza inashika nafasi ya 6 ikiwa na mtaji wa pointi 15 na mwishoni mwa wiki hii watashuka dimbani Nyamagana kumenyana na timu ya Ndanda kutoka Mtwara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.