Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima kwa kupitia Kikao cha Bodi ya Barabara amewaagiza Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA) kuhakikisha wanasimamia ukarabati wa Vivuko na Maegesho kwa wakati ili huduma hiyo muhimu kwa wananchi iweze kurejea kwenye ufanisi.
Akizungumza kwenye kikao hicho leo (Jumatatu Disemba 19, 2022) Mhe. Malima amesema Vivuko Mkoani humo sio anasa wala starehe bali ni huduma muhimu kwa wananchi kutokana na jografia ya uwepo wa makazi mengi kwenye Visiwa hivyo ni lazima kuwe na unyeti katika kuwahudumia.
Ameongeza kuwa vivuko 7 mpaka sasa vipo mikononi mwa Mkandarasi Songoro Marine chini ya usimamizi wa Wakala hiyo hali inayopelekea ugumu kwenye kutoa huduma kwa wananchi kwenye maeneo mengi kwani ongezeko la abiria ni kubwa tofauti na vyombo vinavyotoa huduma.
Vilevile, amewataka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuboresha huduma kwenye uwanja wa Mwanza ikiwemo ukamilishaji wa jengo la kisasa la Abiria na upanuzi wa Barabara ya kutua ndege ili Uchumi ukue kupitia wageni watakaofika Kutalii kwenye hifadhi zinazozunguka kanda ya ziwa kama Serengeti, Burigi-Chato, Saanane, Kigosi na Rubondo.
Akizungumza kwa niaba ya TEMESA, Meneja Vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi Mhandisi Aloyce Ndunguru amefafanua kuwa Taasisi hiyo inaendelea kukarabati vivuko hususani MV Misungwi na maeneo ya maegesho na kwamba taratibu za Manunuzi ya vipuri zinaendelea kwa kushirikiana na Mkandarasi katika kuhakikisha wanakamilisha kazi.
Meneja Mradi kutoka Kampuni ya Songoro Marine William Basiga amesema pamoja na ucheleweshaji wa makabidhiano ya kazi na malipo, kampuni hiyo imejipanga kukamilisha Ukarabati wa vivuko hususani MV Misungwi ambapo tayari wameagiza injini zinazotarajiwa kuingia mwezi januari 2023 ili warejeshe huduma mara moja kwa wananchi.
Aidha, kikao hicho kimewataka pia Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kufuta Ada ya Shilingi 400 wanayotozwa abiria kwa kuingia na kutoka kwenye kivuko cha Buchosa tofauti na ada ya kuvuka wanayotozwa kwani zinawaumiza wananchi kwa kubebeshwa mzigo.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa Mhandisi Paschal Ambroce amesema hali ya Mtandao wa Barabara kwa asilimia 21.7 ni nzuri hadi na kwamba jumla ya Tshs. Bilioni 16.7 zimetengwa kutengengeneza Kilomita 1,355.88 na Madaraja 5 ndani ya mwaka 2022/23.
"Katika mwaka wa fedha 2021/22 Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) tulikua na
jumla ya miradi 99 kati ya miradi hiyo 92 imekamilika na Miradi 7 ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji kama miradi kiporo ambapo jumla ya Bilioni 27.23 zimetumika" Amesema Meneja wa TARURA Mkoa, Mhandisi Goodluck Mbanga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.