Wakazi wa Jiji la Mwanza na vitongoji vyake leo wameshuhudia uzinduzi wa aina yake uliofanywa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Adam Malima wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa kufyatuliwa Fataki 11 zilizosambaza angani miale ya rangi mbalimbali.
Uzinduzi huo uliofanyika kwenye Daraja la Furahisha,Mhe Malima amewakumbusha Wakazi wa Mwanza kutoa ushirikiano wa dhati kwa Makarani wa Sensa watakaoingia kwa kila Kaya ili kukamilisha zoezi hilo la kuhesabu watu.
"Naamini wote tumeelimika vya kutosha kuanzia wahusika wa zoezi hilo yaani Makarani na sisi tutakao hesabiwa,kazi hii ikifanyika kikamilifu faida yake inarudi kwetu kwa kurahisishiwa mipango yote ya Maendeleo" amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Amesema Maendeleo kama kujengewa Shule,Barabara,Hospitali,kupatiwa huduma bora za maji, yote yatapatikana kutokana na ukamilifu wa Sensa ya Watu na Makazi.
Mhe Malima ameonesha Imani kubwa kwa wakazi wote wa Mkoa wa Mwanza kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa na Mkoa huo kuwa mfano miongoni mwa Mikoa mingine hapa nchini.
Katika uzinduzi huo Wakazi wa Jiji la Mwanza wamepata fursa ya kushuhudia hotuba ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa Wananchi kuhusu Sensa ya Watu na Makazi inayofanyika leo nchi nzima kwa wale waliolala ndani ya mipaka ya Tanzania.
Mkuu huyo wa Mkoa katika uzinduzi huo ameambatana na baadhi ya Viongozi waandamizi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala, Katibu wa CCM Mkoa Julius Peter, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama,na Wakuu wa Idara mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.